2014-10-07 14:29:20

Papa: Biblia isomwe kila siku na zaidi Jumapili ndani ya familia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili wakti wa sala ya malaika wa Bwana alikumbusha juu ya ufunguzi wa Sinodi maalumu ya Maaskofu , Kwamba, Maaskofu wanaotoka pande zote za dunia, kwa muda wa wiki mbili watajadili changamoto za kichungaji kwa familia katika mtazamo wa Kazi za kichungaji na uinjilishaji.

Papa aliangalisha pia katika liturjia ya Jumapili, akisema ilionyesha picha ya shamba la mizabibu, kama ishara ya watu, wanaochaguliwa kulihudumia Kanisa, kama shamba la mizabibu lenye kuhitaji watu kulitunza kwa upendo, subira na uaminifu.

Na ndivyo hivyo Mungu anavyofanya kwa watu wake walioitwa kuwa wachungaji. Kutunza familia ya watu wa Mungu, ni kufanya kazi katika shamba la Bwana ili shamba hili lipate kutoa matunda ya ufalme wa Mungu (Mt 21,33-43), Lakini ili familia ipate kutembea vema , kwa imani na matumaini, inapaswa kulishwa Neno la Mungu, na ndiyo maana ni furaha kuona ndugu wa familia wa Mtakatifu Paulo "Paulini", wametaka kugawa Biblia katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na sehemu mbalimbali

Papa aliongeza kwamba, wanafanya ishara hiyo kwa ajili ya kuadhimisha siku ya mwanzilishi wao wa shirika Mwenye Heri Giacomo Alberione, mtume shupavu katika mawasiliano.

Kwa namana hiyo wakati Sinodi imefunguliwa kwa ajili ya familia, kwa msaada wa Wapaulini, Papa anasema ina maana “Kila familia iwe na Biblia”Lakini isiwekwe pemebeni mwa kabati tu, bali iwe mkononi daima, isomwe kila siku, iwe na kibinafsi au kwa pamoja mke na mme,au kama familia wazazi na watoto, wakati wa usiku, na zaidi siku ya Jumapili. Ni kwa njia hiyo familia itakua, na kutembea na mwanga na nguvu ya Neno la Mungu.

Na mwisho, Papa aliwaalika wote kusindikiza kwa sala, kazi ya Sinodi, kwa maombezi ya Bikira Maria. Aliwakumbusha kuungana kiroho katika maombezi kwenye Madhabahu ya Pompei kama utamaduni wa sala kwa mama Maria wa Rosari, azijalie amani familia na Ulimwengu mzima.

Vile vile baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa kwa kifupi alizungumzia kutangazwa kwa Mwenye Heri Sr Maria Teresa Demjanovich wa Marekani wa shirika la Upendo la Mtakatifu Elizabeth, siku ya Jumamosi Oktoba 4, akisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa ajili ya neema ya Mungu kwa Mtumishi wa Kristo aliyeishi kwa kina maisha ya kiroho.

Aliwasalimia mahujaji wote waliotoka nchini italia na pande zote za Dunia, na hasa wanafunzi kutoka nchini Austraila, Ujermani, Jordan,Chama cha Mtakatifu Giovanna de Mathsa, na waamini kutoka Parokia za Mtakatifu Paulo uko Bergamo italia. Mahujaji waliofikia kwa baiskeli kutoka Milan akimkumbuka Mtakatifu Gianna Beretta Molla Matakatifu na mama wa familia na mtoa ushuhuda wa Injili ya Maisha, na waliwatia moyo kuendeleza na ushuhuda wao kwa mshikamano kwa watu walio wadhaifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.