2014-10-03 16:00:14

Rasimu ya Katiba Tanzania yapitishwa


Bunge Maalum la Katiba (BMK), Alhamis lilipitisha Rasimu ya Katiba ya Tanzania, kwa mujibu wa kura zinazotakiwa kiasi cha theluthi mbili ya kura zote kutoka upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar.

Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashilillah, alitangaza hilo wakati wa kukamilisha Mkutano wa siku mbili wa BMK , uliohudhuriwa na wajumbe wote wa Bunge hilo, kutoka Zanzibar walikuwa 219 na Tanzania Bara wakiwa wajumbe 411.

Na kwamba , ili kukidhi matakwa ya kisheria ya kupatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe wote, Zanzibar ilitakiwa kupata kura za ndiyo 146 na Tanzania Bara ilipaswa kupata kura za ndiyo 274.

Taarifa iliyo tolewa na vyombo vya habari inaeleza kwamba, kwa upande wa Zanzibar ni wajumbe 154 ndiyo waliopiga kura na wajumbe 65 hawakupiga kura, huku waliopiga kwa upande wa Tanzania Bara wakiwa ni 335 na ambao hawakupiga kura ni 76. Na kwamba, kila sura na Ibara zilizopigiwa kura, ziliweza kupata theluthi mbili ya kura zote za wajumbe na hivyo kukidhi matakwa ya kisheria.

Habari zaidi kutoka mkutano huo, zinaendelea kusema, baada ya ushindi huo kutangazwa , ukumbi wa mkutano ulilidima kwa shangwe, vifijo na vigelegele kutoka kwa wajumbe wa Bunge hilo. Na baada ya wajumbe hao kutulia, Mwenyekiti wa BMK, alimkaribisha Mheshimiwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ili atoe hoja juu ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa. Na pia baadhi ya wajumbe walipewa nafasi ya kuzungumza, akiwemo Mbunge wa Wawi, Mheshimiwa Mbunge Hamad Rashid, aliye eleza kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Watanzania wamepata fursa ya kukaa pamoja kuandika katiba, hivyo akawaomba watanzania kutumia fursa hiyo kuipokea na kuikubali Rasimu ya Katiba, ili kudumisha amani na utulivu wa taifa.

Na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Mheshimiwa Mbunge Stephen Wassira, yeye alitoa pongezi kwa watu wote walifanikisha upatikanaji wa Katiba inayopendekezwa, lakini pia anawapa pole wale ambao walikuwa hawalali kwa kuitakia mabaya BMK, kwamba imeshindwa. Na amewataka Watazania sasa kujenga umoja zaidi , hasa wakati wa kupiga kura ya maoni, kwa ajili ya kuipa uwezo Katiba mpya kuanza kutumika.

Wengine waliopewa nafasi za kutoa maoni yao ni Sheikh Thabit Jongo, Anna Abdallah, John Cheyo, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Paul Makonda na Jeska Msambatavangu.

Rasimu iliyopitishwa itakabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamde Shein, Oktoba 8, mwaka huu.








All the contents on this site are copyrighted ©.