2014-09-27 16:04:23

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 26 YA MWAKA A, 28SEPTEMBATAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 26 YA MWAKA A, 28SEPTEMBA
Karibuni mpendwa tusali pamoja tukiongozwa na neno la Bwana likitualika kubadili maelekeo yetu mabaya na kumrudia Bwana. Mwaliko huu tunaupata katika mahubiri ya nabii Ezekieli katika somo la kwanza akisema wajibu wetu ni kuacha dhambi na kuanza maisha mapya, maisha yaliyojaa heri na fanaka nyumbani mwa Bwana. Na anawaonya wale wema watakapoghairi njia ya haki, anguko lao ni kubwa na watakufa katika anguko hilo.

Nabii Ezekieli anatoa mafundisho haya wakati Waisraeli wako utumwani Babeli, wanateseka na kulalamika wakisema, kwa sababu ya dhambi za mababu zetu tunateseka hapa ugenini. Kumbe nabii Ezekieli anaibuka akiwaambia kuwa kila mmoja wao anawajibika katika makosa yake kwa hivi suala la baba zao kutenda dhambi si la msingi, la msingi ni kuacha njia mbaya na kumrudia Bwana. Nasi hivi hivi twaweza kubaki katika kulalamika juu ya makosa ya wengine tukasahau wajibu wetu wa toba katika maisha yetu ya imani. Tunapaswa kukumbuka kila siku juu ya wajibu wetu wa ubatizo na si juu ya dhambi za wengine.

Mtume Paulo anaendelea kuwaasa Wafilipi kukaa katika pendo la Bwana yaani kukwepa ugomvi na ushindani unaokuza ubinafsi na majivuno, badala yake wakue katika unyenyekevu na mapendo ya jirani yanayomweka mwenzangu mbele yangu daima. Kwa kukuza mapendo tunafuata mfano wa Kristu aliyekuwa yunamna ya Mungu lakini alijinyenyekeza na kujifanya hana utukufu akatwaa namna ya mtumwa, akawa mwanadamu na mwisho ametii mpaka kufa mauti ya msalaba. Matunda ya unyenyekevu wa Kristu ni kwamba Mungu alimwadhimisha mno na sasa kila goti linapigwa mbele yake. Si goti tu linalopigwa mbele yake bali wokovu wa ulimwengu. Mpendwa msikilizaji, Sisi leo hatuna budi kufuata kiuaminifu mfano huo wa Kristu mkombozi na hasa tunapotangaza neno la Mungu, tunapotunza familia zetu, tunapoimarisha vyama vya kitume na aina nyingine ya utume katika Kanisa na nchi kwa ujumla. Hatutadaiwa mambo makubwa bali matendo yaliyojaa unyenyekevu.

Mwinjili Mathayo anatufundisha umuhimu wa kutenda kwa moyo na si kwa maneno akitupatia mfano wa watoto wawili wa baba mmoja. Mtoto mmoja anaambiwa na baba yake kwenda shambani na anaitikia kwa nguvu kuwa anaenda na baadaye haendi. Mtoto wa pili anaambiwa nenda shambani na anasema siendi, na baadaye anapiga moyo konde anatubu na anakwenda shambani. Kati ya hawa yule wa pili anatenda kwa moyo wa toba anapiga hatua kurudi kwa baba yake na hivi anatimiza mapenzi ya baba yake.


Mpendwa, kumbuka toba ni ya maana katika maisha ya kikristu na hata katika maisha ya kawaida. Kijana huyu aliyetubu anatudhihirishia uwepo wa nafasi katika nyumba ya Baba kwa ajili ya watenda dhambi wanaotubu, na hivi kinyume chake ni kwamba wale wote wanaojisikia kiburi na wema yaani wale wanaosema tunaenda shambani na baadaye hawaendi hawana nafasi katika nyumba ya Bwana. Kwa ujumla Mungu anatutaka mabadiliko ya moyo yaliyo makamilifu (total conversion). Anatutaka tushike imani ambayo ni tendaji na tambuzi kwa mapenzi ya Mungu. Imani ambayo humwona Mungu aliye upendo na si mfanya biashara ambaye hucheza na faida. Imani ambayo humwona Mungu ambaye mawazo yake ni ya juu kuliko mawazo ya kibinadamu.


Mpendwa, ni wakati wetu kutafakari na kuona zaidi namna tutakavyoendesha maisha yetu ili yaambatane na mapenzi ya Mungu.Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps
All the contents on this site are copyrighted ©.