2014-09-26 15:44:37

Papa-imani yenu isiwe kama povu zuri la sabuni lenye kuonekana na mara hutoweka


(Vatican Radio) Wakati wa Ibada ya Misa ya mapema asubuhi Alhamisi, katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta, Papa Francisco alitahadharisha dhidi ya ubatili , unaoweza kutuweka mbali na ukweli na kutufanya tuonekana kiimani kama “povu la sabani.” Papa alieleza na kutoa msisitizo kwa Wakristo wanapotenda wema, lazima kuepuka kila kishawishi cha kutangaza wema huo.

Homilia ya Papa ililitazama somo kutoka Kitabu cha Mhubiri juu ya ubatili , akisema, ubatili si tu majaribu kwa ajili wapagani lakini pia kwa Wakristo, na watu wenye imani. Na kwamba, Yesu, mara nyingi alikemea tabia ya kutenda mema kwa nia za kujionyesha na majigambo na kujisifia mwenyewe. Aliwaonya walimu wa sheria, wasitembee mitaani kwa mavazi ya kifahari na anasa. pia alifundisha wafuasi wake wakati wanaposali " wasijionyeshe kwa watu, bali waingie mahali pa faragha.

Papa ametoa msisitizo kwamba, ni lazima kufanya hivyo, na kuongeza, hata wakati wa kusaidia maskini, inapaswa kuwa kitendo cha faragha na si kupiga sauti za tarumbeta juu yake, kwa kuwa Baba wa Mbinguni huyaona yote hata ya sirini.


Papa alieleza na kutoa mfano wa matajiri wanaosaidia kanisa ambao huandika hundi nono kwa kanisa huku wakitangaza kwa kujisifia “Tazama, mimi nimetoa hundi hii kwa ajili ya kazi ya Kanisa”, au wale wenye kusema mimi shida naAskofu, au Padre au watawa,lakini kumbe majingambo ya mtu huyu ni kutokana na utajiri wake, lakini kiimani yuko mbali na Mungu na yuko mbali na kanisa. Kufanya hivyo ni bure. Vivo hivyo wakati wa Mnapofunga, Bwana anasema, msivae sura za simanzi na huzuni, ili kila mtu atambue kama mmefunga. Bali onekana mtu wa kawaida. Fanya toba kwa furaha, ili asiwepo mtu mwenye kutambua kama umefunga. Kupiga debe kama umefunga, huo ni ubatili. Ni kujionyesha, ni maisha ya kujionyesha.

Papa alikemea hilo , na kusema wapo Wakristo wanaoishi kwa njia hiyo ya kujionyesha, njia ya ubatili, inayoweza kufananisha na maisha ya tausi ambaye wakati mwingine huutandaza uzuri wa manyoya yake, na mara huyakuja na uzuri huo kutoweka. Waamini wa aina hiyo ni wale ambao hujitangaza "mimi ni Mkristo bora au mimi nina uhusiano mzuri na Padre, au Askofu, au kwamba familia yangu ni ya Kikristo. Ni mahodari wa kujivuna. Lakini, kumbe imani yao ni mbali na Yesu anavyotutaka kufanya.

Papa alieleza na kumtaka kila muumini kabla ya majigambo hayo kwanza ni kujiuliza, je maisha yangu pamoja na Bwana yakoje? Na kwa jinsi gani u karibu na Bwana katika maombi? Na je maisha yako katika matendo ya huruma, yakoje, hasa katika kwenda kutembelea wagonjwa na kusaidia wahitaji? Je wafanya hivyo kwa sababu za kutafuta ufahali na faida binafsi? Ukweli aliongeza, Yesu anatuambia sisi lazima kujenga nyumba zetu, juu ya mwamba wa ukweli, Yesu alionya kwamba" bure kujenga nyumba zetu juu ya mchanga, na nyumba ambayo iko juu ya mchanga, huporomoka mara kwa majaribu kidogo kwa sababu hakuna uwezo wa kuhimili mapigo ya majaribu.


Papa aliendelea kueleza jinsi Wakristo wengi wanaishi kwa ajili ya kujionyesha, ambao imani yao kwa Kristo ni kama povu la kupendeza la sabuni, ambalo huonekana kwa kishindo na mara hutoweka. Aliongeza, hata katika jinsi ya misiba inavyoendesha na makaburi yanayojengwa leo hii, ni ubatili mtupu. Hakuna maana ya kuwa na mbwebwe nyingi, kama Mtumishi wa Mungu Paulo VI alivyosema, ardhi ni wazi, inatusubiri sisi sote, huu ni ukweli wa mwisho wetu. Kama ndivyo, kuna haja gani ya kujivunia jambo? Mimi nimefanya kile nimefanya hiki, nimefanya mambo makubwa, hakuna sababu ya kujivuna maana yote ni ubatili, ni ubatili, uongo, ubabe, na ni kujidaganya mwenyewe.
All the contents on this site are copyrighted ©.