2014-09-26 12:24:01

Kardinali Pietro Parolini : Watu wote wabebe jukumu la kulinda mazingira.


(Vatican Radio) Katika Mkutano Mkuu wa 69 wa Umoja wa Mataifa unaondelea huko mjini New York Marekani, Katibu wa Vatican Kardinali Pietro Parolini ametoa ujumbe wake kama mwakilishi wa Papa katika Mkutano huo.

Amesema, ni bayana kwamba, mabadiliko ya tabianchi hayaangalii tu sayansi, mazingira, siasa na uchumi , bali yanagusa masuala yote hata maadili ya mwanadamu, kwa sababu jamii ndiyo inaathirika na hasa watu masikini kati yetu. Vatican mara nyingi imesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika utendaji ili kwamba kila mmoja aweze kubeba jukumu la kulinda na kuthamini viumbe kwa ajili ya uzuri wa dunia kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Vilevile alikumbusha kwamba , Tangu mwanzo wa utume wake, Papa Francisko amekuwa akisisitiza suala la kulinda mazingira yetu. Lakini bado kuna matumizi mabaya ya mazingira, badala ya kutumika vema, yanachakazwa, kunyonywa na kusababisha madhara makubwa.

Utafiti wa kisayansi unathibitisha kwamba tangu nusu ya miongo ilioyopita kumekuwa na ongezeko la joto kupita kiasi. Ni tatizo kubwa na hasa kwa madhara ya sekta ya jamii inayo ishi katika mazingira magumu na zaidi itakuwa pia kwa vizazi vijavyo. Tayari inadhihirika gharama za uchumi, na tatizo ongezeko la hewa chafu ya ukaa angani ni matokeo ya utendaji mbovu wa shughuli za binadamu.

Kardinali Parolini anabainisha, katika kukabiliana na hatari za gharama hizi, ni busara kuchukua hatua za kuzuia , ambazo zinahitaji uamuzi sahihi wa kutenda ukizingatia pia mazuri ya siku zijazo. Hili ni hitaji na uwajibikaji mkubwa katika dhamira ya kisiasa na kiuchumi kwa Jumuiya ya Kimataifa , ambayo pia Vatikan inatoa mchango wake ikiwa inatambua kwamba “zawadi ya maarifa inasaidia kutoangukia katika dimbwi la mafanikio yasiyo jali uharibifu.

Kupambana na tatizo la ongezeko la joto duniani linahitaji umakini siyo tu kuimarisha, au kukuza mchakato wa kisiasa katika ngazi ya kimataifa, lakini pia ni kuwa waaminifu katika ahadi zetu zinazodai mabadiliko katika utendaji na kugundua zaidi juu ya maadili msingi ambao familia na jamii nzima ya binadamu inaweza kujengwa juu yake.

Vatican inalenga katika utendaji wenye uwajibikaji, na inatambua kuwa Jumuiya ya kimataifa itaweza kuongozwa na utendaji adilifu, kwa mujibu wa kanuni ya mshikamano na manufaa ya wote, katika utambuzi wa kuheshimu msingi ya haki kwa kila binadamu. Huu ni wajibu kwa kila binadamu, unaotakiwa kutekelezwa kwa manufaa ya wote, na kwa ajili ya kuboresha na kupatia sura mpya, mambo yote ya uchumi na siasa.(Evangelii Gaudium, 203)








All the contents on this site are copyrighted ©.