Katekesi ya Papa kwa mahujaji wageni kwa Jumatano hii mjini Vatican, imetafakari
safari yake ya kitume katika Mji Mkuu wa Tirana Albania. Ziara ya siku moja lakini
aliyoitaja kwamba, ilijaa utajiri mkubwa wa upendo na mshikamano kati ya Jimbo Takatifu
na nchi ya Albania.
Katika Maelezo, Papa Francisco amesema, alikwenda Albania,
kuonyesha mshikamano wake wa karibu na Kanisa zima na watu wa Albania, taifa ambalo
kwa muda wa miaka mingi, liliteswa na kushamiri kwa ukana Mungu , na unyama wa serikali
isiyojali uwepo wa Mungu. Baada ya kuangushwa kwa mamlaka hayo, sasa taifa linahitaji
kupewa moyo, kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi nyingi za kuijenga upya jamii, ili
iwe ni jamii yenye kupenda amani na kuheshimiana na kushirikiana katika huduma, kwa
ajili ya manufaa ya wote.
Papa ameonyesha kufurahi na kumshukuru Mungu, kwa
uwepo wa roho ya mshikamano na mazungumzo kati ya jamii Albania licha ya tofauti
za kidini na kitamaduni. Anamwoba Bwana, ili taifa hili lisonge mbela na roho huyo,
na kamwe lisirudishwe nyuma katika mateso makali ya ukana Mungu. Papa alieleza kwa
kuurejea Mkutano wake na viongozi wa dini mbalimbali, ambamo aliweza mwenyewe kuushuhudia
moyo huo wa kuheshimiana na kushirikiana, uliojengwa juu ya utambulisho wa kila mmoja.
Papa Francisko, ameendelea kusema akiwa pamoja na ndugu zake katika Kristo wake kwa
waume, waliweza kutoa heshima zao kwa ushuhuda wa kishujaa wa mashahidi wengi wa imani,
ambao mateso yao sasa yanatoa matunda ya taifa kuzaliwa upya kiroho. Kwa ajili hiyo,
Papa ametoa mwaliko kwa Wakristo wote, kuwa chachu ya wema, upendo na maridhiano katika
jamii ya Albanian. Na ameomba msaada wa Mama Yetu wa Shauri Jema, Mungu aridhie kuendelea
kuwasha mwamko na moto wa kujenga jamii ya haki, amani na Mshikamano, kwa Walbania
wote..
Baba Mtakatifu francisko alikamilisha tafakari yake kwa kusalimia makundi
mabalimbali ya mahujaji na wageni waliofika kumsikiliza wakiwemo wanafunzi wapya waliojiunga
katika masono kwenye Taasisi ya Uingereza, kama wanafunzi wanao wania kuwa Mapadre.
Papa aliwahakikishia wanafunzi hao kwamba, kiroho yu karibu nao,hasa wakati huu wanapoanza
mwaka wa kwanza wa masomo kwa ajili ya Upadre. Pia alitaja makundi mengine yanayozungumza
lugha ya Kiingereza wengi wakiwa kutoka Uingereza, Ireland, Scotland, Denmark, Norway,
Uholanzi, India, China, Japan, Kenya, Australia, New Zealand, Canada na Marekani.
Kwao wote aliwaombea furaha na amani ya Bwana Yesu. "Mungu awabariki"!