2014-09-22 14:05:58

Papa asisitiza udumishaji wa urithi wa mashahidi na mshikamano- Albania


(Vatican Radio) Baba Mtakatifu Francisko Jumapili jioni alikamalisha ziara yake ya kitume ya siku moja katika mji wa Tirana, Mji Mkuu wa Albania,taifa la zamani la Kikomunisti. Ziara iliyomchukua Papa saa 11, ambayo aliianza mapema asubuhi Jumapili na kurejea Vatican majira ya usiku. Taarifa zinasema, licha ya kuwa fupi , ilikuwa ni ziara muhimu, iliyolenga madhari kuu mbili, Urithi wa shuhuda za mashahidi na umuhimu wa amani kuwepo kwa ajili ya ushirikiano na mshikamano wa utendaji kwa manufaa ya watu wote.

Katika hotuba zake, Baba Mtakatifu aliwarejesha Waalbania kutafakari mara ingine kwa makini, ukweli na maana ya ushuhuda ulioachwa na mashahidi wa Albania hasa waliouawa wakati wa utawala wa ukana Mungu wa kikomunisti wa siku za nyuma, katika taifa hilo. Alisema, leo hii sauti iliyo nyamazishwa ya mashahidi wa Kanisa Albania, inaongea kwa sauti kubwa, kuushuhudia utamaduni wa imani kwa taifa, imani ambayo ni mwamba imara , na juu yake inawezekana kujenga hali bora ya maisha ya nchi ya Albania ya siku za usoni.

Ni ujenzi wa hali bora ya baadaye, ya maisha yenye maelewano na mshikamamo wa karibu zaidi ya kuheshimiana wote, ambayo imekuwa ni sifa ya Albania tangu kuanguka kwa Ukomunisti. Papa alieleza, zaidi ya uzoefu wa kubaki katika eneo moja, kuishi katika hali mchanganyiko kwa amani na maridhiano kunahitaji kuheshimiana mmoja kwa mwingine, kuheshimu hadhi utu wa mtu, mzizi wa lazima katika kuwa na imani kwa Mungu, Muumba wa kila kitu.

Aliongeza, raia wa Albania, ni wazi wana hisia kali za zamani, hasa historia ya kutisha ya miongo kadhaa ya nyuma iliyopita hivi karibuni.Historia ambayo leo hii imekuwa ni sababu kwa Wakatoliki wa Albania, wanaonea fahari wafia dini wao , ambao walimtegemea Mungu,watu waliosimama imara katika Imani yao.

Na hivyo , Paapa Francisko aliyoonyesha imani yake kwamba, matumaini ya watu wa Albania kwa ajili ya siku zijazo, sasa yanahamasishwa na kipindi cha mpito kuelekea demokrasia kamili , ambayo bado kupatikana kikamilifu . Papa alitaja hisi za wasiwasi kwa ajili ya baadaye na , hofu kwamba, ahadi ya mapambazuko mapya kwa Albania, inaweza isifikie matarajio. Papa ameatia moyo watu wa Albania wasikatie tamaa ujenzi wa taifa bora, na iwapo wana mashaka na siku zijazo, inawapasa kusimama imara katika imani inayorishwa na tumaini jema kwa siku za baadaye, hasa kupitia njia ya umoja na ushirikiano wa kitaifa.

Papa Francisko, aliwaelekea hasa vijana na kuwasisitiza kwamba, hali ya baadaye ya taifa hilo, haiwezi kujengwa kwa ahadi tupu, au ubinafsi na choyo. Ni lazima kujengwa juu ya upendo na kuheshimiana, ambavyo ndani yake mmefumbatwa ujumbe wa wokovu wa Yesu Kristo. Ni ujumbe wa matumaini mema kwa taifa la Albania, na kamwe wasikate tamaa, Papa aliwasisitiza.
All the contents on this site are copyrighted ©.