2014-09-21 13:26:57

Papa amepeleka zawadi ya amani kwa taifa la Albania


Jumapili hii 21 Septemba 2014, Baba Mtakatifu Francisco, amefanya ziara ya Kitume katika mji wa Tirana Albania, ambako ameongoza Ibada ya Misa katika uwanja wa Mtakatifu MamaTereza.Katika homilia yake, amehimiza raia wa Albania kuwa na imani na matumaini, kuifungua mioyo yao kwa Kristo, na katika kutimiza wajibu wao kwa Kanisa na maisha ya kijamii.

Hii ilikuwa ni mara ya Pili kwa Albnania kutembelewa na Papa. Ziara ya kwanza ilifanywa na Papa Yohane Paulo 11 hapo tarehe 25 April, 1993, ikiwa imepita miaka miwili baada ya kuagushwa kwa utawala wa kidikteta na kikomunisti.

Wakati wa Ibada katika homilia yake Papa Francisko, amekumbusha mateso makali waliyo yaishi mashahidi wafia dini wa Albania, Wakatoliki, Waotodosi na Waislamu.

Na pia aliangalisha katika ukweli halisi kwamba ,taifa la Albania bado ni changa, na hivyo akahimiza pamoja na kutosahau uchungu walioupita miaka ya nyuma,pia ni muhimu kusonga mbele na mabawa ya matumaini.

Na akitafakari masomo ya Jumapili hii, Papa amekumbusha jinsi Yesu alivyounda jumuiya ya Mitume wake 12 na wengine 72 na kuwatuma wawili wawili kutangaza Neno la Mungu. Papa ameziita Jumuiya hizi kuwa , jumuiya ya kimisionari , Jumuiya iliyokuwa katika njia , ikijishughulisha na kazi za kutembelea nyumba hadi nyumba kutangaza Injili, wakianza na salaam maalum na zawadi ya amani “ amani katika nyumba hii”.

Na hiyo ndiyo ilikuwa nia kuu ya Ziara ya Papa kwa taifa la Albania ni kufika na kuiambia kila kaya ya Albania “Amani katika nyumba hii , na Amani katika kila moyo wa raia wa Albania”.

Papa alieleza, katika moyo wa kazi za mitume 72 pia inaonyesha uzoefu wa kazi za kimisioanri kwa jumuiya za Kikristo za nyakati zote. Bwana Mfufuka na aliye hai, hakuwatuma tu mitume 12, lakini Kanisa lote , na kila mbatizwa kuifanya kazi hii ya kutangaza Injili kwa watu wote.

Papa alirejea jinsi siku za nyuma, milango ya Albania ilivyokuwa imefungwa na minyororo ya ukana dini na madhulumu, ambavyo viligandamiza uhuru wa kidini.Watu waliokuwa na woga katika kuutangaza ukweli na uhuru, walifanya kila lililowezekana kumzuia Mungu kuingia katika mioyo ya watu, walimweka Yesu nje ya mioyo ya watu, na Kanisa katika historia ya nchi hiyo , licha ya kuwa kati ya nchi za mwanzo zilizo pata bahati ya kupokea mwanga wa Injili.

Baba Mtakatifu aliendelea kuitazama hali halisi ya Albania akisema, imekuwa ni nchi ya Wafia dini , yenye kuwa na madhulumu makali dhidi ya Wakatoliki ,Waotodosi na Waislamu pia. Na hivyo Papa ametoa mwaliko wa nguvu kwa Wakristo, Maaskofu , Mapadre , Watawa na waamini walei,wasikubali kuinamia unyanyasaji na vitisho vya utawala mbovu. Papa amewataka wawe imara kama ulivyokuwa imara ule ukuta wa Scutari , ambao ni alama ya Wakatoliki wafia dini katika eneo hilo ambao walimwanga damu yao kama wana kondoo na kuchipuka kama ua la sala.

Papa amewatia moyo Waalbani akwamba, leo hii milango ya Albania i wazi na inaendelea kukomaa katika hatua mpya za utendaji wa kimisionari kwa watu wote wa Mungu.Na hivyo kila mbatizwa anayo nafasi yake katika kazi na utume wa kuinjilisha, na utendaji wa jamii kwa manufaa ya wote. Papa ametoa wito kwa kila mmoja kusikiliza wito wake na kuitikia kwa moyo wa ukarimu, kwenda na kuitangaza Injili, kuwa shahidi wa upendo, na kuimarisha urithi wa mshikamano kwa ajili ya kuboresha hali ya maisha yenye haki zaidi na udugu kwa watu wote.

Papa Francisco kisha, alikigeukia kizazi kipya cha Vijana na kuwataka wajilishe kwa Neno la Mungu na kutembea na Kristo mioyoni mwao , kwa kuwa Neno lake la Injili huionyesha njia ya maisha. Aliwahakikishia kwamba,kuwa na Imani kwa Yesu,ni kuchagua maisha ya furaha yanayong’arishwa kwa kukutana na Kristo na kutoa maana ya maisha ya kila binadamu, awe mke au mme.

Baba Mtakatifu alihimiza mahusiano katika kazi za kichungaji na mwendelezo wa tafiti kwa ajili ya kuhamasisha mabadiliko mapya chanya katika Kanisa na jamii nzima. Na kwa namna ya pekee amewahimiza Vijana kutoogopa kutoa jibu kwa ukarimu kwa Kristo anayewaita kumfuata katika utumishi wa Mungu na kwa jamii. Papa alimetolea sala zake ili kwamba watu wengi wanaume na wanawake waweze kuusikia wito huu katika mwanga wa Injili na neema za Sakramenti.

Nyakati za adhuhuri, baada ya Ibada ya Misa,Papa aliongoza sala ya Malaika wa Bwana. Papa katika hotuba yake, alirudia kutoa ujumbe kwa vijana,ambamo aliwataka watafute msaada wa maisha kwa Yesu Kristo. Alikumbusha anayejijenga kwa Krsito anajijenga katika mwamba imara. Yesu mwenye kutufahamu vyema pale tunapokosea,hatuhukumu lakini husema, “nenda sasa na usifanye dhambi tena(Gv 8,11). Kwa nguvu ya Injili na mfano wa Wafia dini, tunapata kuelewa kusema hapana kwa kishawishi cha fedha, Hapana kwa uhuru wenye ubinafsi, hapana katika kuwa tegemezi na ghasia.Badala yake ni kusema ndiyo katika utamaduni wa kukutana, na ndiyo katika uzuri wa kutenda wema, ndiyo katika kuwa na furaha kuu ya kina ya moyo.Ni ndiyo katika kuwa aminifu hata katika vitu vidogo vidogo.Na kwa namna hiyo , inawezekana kuijenga Albania iliyo bora zaidi na dunia nzuri zaidi.

Papa alikamilisha hotuba yake kwa kumrejea Mama Yetu wa Shauri jema wa Scutari,akiomba msaada wake kwa Kanisa la Albania na watu wote wa Albania na hasa kwa ajili ya familia, watoto na wazee. “Mama Maria ,awaongoze katika njia ya kutembea pamoja naMungu,kuelekea tumaini lisilofadhaisha”.
All the contents on this site are copyrighted ©.