2014-09-18 07:56:18

Familia za Kikristo ziwe chumvi na mwanga wa mataifa


Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ameitaka familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Musoma kuwa kweli mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia kwa njia ya maneno na matendo yao yanayodhihirisha imani tendaji. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo. Askofu mkuu Padilla anasema Kanisa ni familia moja kubwa inayoundwa na waamini wenye dhamana na nyadhifa mbali mbali. Ni Jumuiya kubwa inayowajibika mbele ya Mungu na wanadamu.


Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, familia haina budi kupwa kipaumbele cha kwanza, kwa kutambua kwamba, familia ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, dhana inayopaswa kutekelezwa na waamini walei katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Ili kutekeleza dhamana hii, kuna haja kwa Mama Kanisa kuwajengea waamini walei uwezo wa ukabiliana na majukumu yao kikamilfu kwa njia ya mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, lengo ni kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili.


Askofu mkuu Padilla amewataka waamini wa Jimbo Katoliki la Musoma kuwa kweli ni mabolizi wema na waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya maneno na matendo yao yanayojikita katika ukweli, haki, amani na upataniso. Famili ya Mungu Jimbo Katoliki la Musoma itambue wajibu wake kwamba ni Jumuiya ya Kimissionari inayotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanaymwilishwa katika imani tendaji, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.


Waamini watambue kwamba, wao ni Kondoo wanaotumwa kati ya mbwa mwitu, lakini hawana sababu ya kuogopa ikiwa kama watashikamana na kuandamana na Kristo katika maisha yao. Vita n mahangaiko ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, silaha kuu ni umoja na mshikamano kwani Kristo ana uwezo wa kuwaokoa kutoka katika shida na magumu wanayokabiliana nayo.


Familia ya Mungu haina budi kujikita katika kutafuta mafo ya wengi, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, kwani haya ni mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Dunia imekanganyikiwa kutokana na uwepo wa vurugu, vita na kinzani mbali mbali za maisha, mambo yanayoendelea kumhuzunisha Bikira Maria, hii inatokana na ukweli kwamba, ubinafsi umetawala na mafao ya wengi yamewekwa pembeni. Mstokro yake ni vita, ukosefu wa misingi ya haki na amani. Watu wanashindwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu. Kwa hakika mioyo ya watu wengi imegubikwa kwa giza na ubinafsi.


Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Musoma inapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kuanzia kwenye familia za Kikristo na kuachana na ubinafsi na uchoyo na badala yake mafao ya wengi yapewe kipaubele cha kwanza. Kwa njia ya mfano wa maisha na imani tendaji, Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki Musoma iwe ni mfano bora wa kuigwa kwa kukoleza haki, amani na upatanisho.


Naye Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma akimkaribisha Askofu mkuu Padilla kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mtakatifu Jimbo Katoliki Musoma, alisema, Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Musoma ina hamu ya kumsikiliza Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ii aweze kuwapatia matumaini katika kutekeleza maisha na utume wa Kanisa jimboni Musoma. Jimbo linasali na kumwombea Baba Mtakatifu katika utume wake wa kuliongoza Kanisa la Kristo. Itakumbukwa kwamba, Jimbo la Musoma linaundwa na Parokia 32 kwa sasa.


Monsinyo Aristaric Bahati, Dekano wa Dekania ya Musoma mjini, amemwelezea Balozi wa Vatican nchini Tanzania shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Jimbo Katoliki Musoma katika Udekano wa Musoma mjini, katika azma ya kumhudumia mwanadamu, kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.