2014-09-16 08:26:33

Kanisa la Nyumbani -Uaminifu


Tumsifu Yesu Kristo! Tuhitimishi mfululizo wa mada yetu juu ya uaminifu kama sehemu ya uadilifu wetu. Katika vipindi vilivyopita sote tumetazama kwa rasha juu ya uaminifu na tukahimizana kwa dhati kila mmoja kujijenga katika dhamira ya uaminifu katika mambo yote. Bwana asema “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa”(Lk. 16:10).

Nasi tukijizoesha kukosa uaminifu katika mambo madogo madogo ya kawaida, hata katika makubwa hatutakuwa waaminifu, tutaharibu kazi ndogo na kubwa pia, tutakwamisha maendeleo. Katika ujumla wake, tukumbuke kuwa uaminifu si tu elimu ya kiakili, bali ni sanaa ya kuishi inayopenya maisha yote ya mwanadamu. Hapa tunataka kusema kwamba, kufahamu uaminifu na mafaa yake tu haitoshi, bali yatakiwa kujibidisha kuuishi uaminifu.

Katika sehemu ya mwisho tuone uaminifu katika mambo yamhusuyo Mungu. Sote tunaomsadiki Mungu, tunaongozwa na nidhamu fulani za maisha kadiri ya dini zetu. Kila mmoja ili kutunza uhusiano wake na Mungu, na pia na jamii ya waamini wenzake, anapaswa kuwa mwaminifu. Na huo uaminifu unadhihirika katika uwiano katika ya mafundisho ya imani na yale adilifu na dini zetu na hali halisi ya maisha.

Kupurukusha uaminifu kwa Mungu ni namna ya kusaliti agano letu kwa Mungu na daima madhara yake ni maumivu tu. Bwana mwenyewe asema “watu hawa wananiabudu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami”. Lalamiko hilo la Mungu linadhihirisha ambavyo huwa tunakosa uaminifu. Na nyakati zetu hizi, kukosa uaminifu kwa Mungu kunajidhihirisha ambavyo wengi wetu tunakumbatia imani za kishetani. Na shetani akisha kukukamata vizuri hakuachi hadi amekutwanga baraabara. Uaminifu kwa Mungu unatupatia amani rohoni, uhuru na usalama.

Katika ubatizo wetu, na daima kila tunaporudia ahadi za ubatizo, tunaulizwa swali zito kwamba “unamkataa shetani, na mambo yake yote, na fahari zake zote”? nasi kwa maswali yote hujiku kuwa “namkataa”. Hiyo ‘namkataa’ tunayoitamka tunataka kudhihirisha zaidi imani yetu kwa Mungu, na Mungu peke yake. Lakini kwa uhalisia wake, tunatamka kuwa namkataa, huku tukiwa tumemkumbatia kwa nguvu zetu zote na mioyo yetu yote.

Katika ulimwengu wetu wa leo ulioshetanishwa katika nyanja zote, wapo watu wengi wanaofikiri kuwa hawawezi kuishi wala kupata maendeleo yoyote bila nguvu ya shetani. Hata mambo ya kawaida kabisa ya kutumia akili ya kibinadamu, wapo ambao wanamsadiki na kumtumainia shetani kwa moyo wote. Matokeo yake wanakuwa watumwa wa itikadi za kisheni au itikadi za kishirikina.

Hilo linadhihirisha kwa uwazi zaidi kukosa kwetu uaminifu kwa Mungu, ambaye tulimwapia kumsadiki na kumtumainia. Badala yake tunachanganya Mungu na shetani. Kwa dhambi hiyo hapo hatuwezi kubaki salama. Matokeo yake ndiyo kuhisiana vibaya, mauaji ya vikongwe wasio na hatia (kwa baadhi ya jamii), na kila aina ya wasiwasi na fujo. Huwezi ukawa mwamini wa shetani halafu ukabaki na amani ya kweli. Waamini wote wa shetani, wamejaa wasiwasi, hisia mbaya na virusi vya vurugu daima.

Na wakati mwingine tunajikuta katika hali hatarishi ambapo, uaminifu wetu kwa shetani na ahadi zake unakuwa ni mkubwa na wenye nguvu zaidi kuliko uaminifu wetu kwa Mungu. Mungu kwa njia ya neno lake akitupatia mwongozo wa kufuata, wengi tunaona ni vigumu sana kufuata. Lakini shetani akitupatia sera za kufuata hata kama ni ngumu sana, wanadamu huwa wanajitahidi kwa maumivu aibu zote kufuata kiaminifu. Ndipo hapo tunapoweza kukuta kuna utekelezaji wa vitendo vya kishetani katika jamii zetu. Nguvu ya kufanya hayo maovu makubwa makubwa inatoka wapi? Ni kule kushika uaminifu kwa shetani badala ya kumwa mwaminifu kwa Mungu na neno lake.

Sisi tunataka tujinidhamishe katika uaminifu wa kweli, ili mwisho wa uzima wetu tukaisikie sauti ile ya faraja isemayo “... Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako” (Math. 25.23)

Basi mpendwa msikilizaji tunaendelea kuomba, tunu hii ya uaminifu ifundishwe kwa wote, na sote tujijenge katika uaminifu ili tufikie maendeleo-kusudiwa ya kimwili na kiroho. Kukosa uaminifu kunatutenga na Mungu, kunatutenga na jamii ya watu adilifu. Uaminifu unatupatia kibali machoni pa Bwana na mbele za watu waadilifu. Kutoka katika Studio za Redio Vatikani, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.