2014-09-13 08:15:02

Upendo ni nusukaputi katika kusahihishana makosa-asema Papa


kusahihishana kikweli kidugu kunaweza kuwa kuchungu kwa sababu hufanyika kwa upendo, ukweli na unyenyekevu. Kama wewe huko radhi kusahihishwa na ndugu yako, basi wewe si mtu wa Mungu. Ni maelezo ya Papa Francisco mapema Ijumaa wakati akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta mjini Vatican, kama sehemu ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Jina Takatifu la Maria.

Maelezo ya Papa yalilenga katika somo la Injili ambamo Yesu anawaonya wale wanaopenda kusahihisha makosa madogomadogo ya wenzao na kuwa wachungu kusahihishwa dhambi zao kubwa, " ondoa kwanza boriti katika jicho lako ndipo uweze kuona kibanzi katika jicho la ndugu yako.

Akizungumza juu ya aya hizo za Injil, Papa Francisko pia alifanya rejea katika mahubiri yake ya nyuma, juu ya ndugu kurekebishana, akisema ni muhimu kwa ndugu wapokosa, wakosolewa au wasahihishwe lakini upendo. Alitolea mfano, ni vigumu kwa daktari kufanya upasuaji katika mwili wa mtu bila nusukaputi. Ni jambo lisilowezekana vinginevyo mgonjwa atakufa kwa maumivu. Vivyo hivyo , upendo ni nusukaputi inayomsaidia mtu kupokea tiba na kukubali kusahihishwa,ni huduma na katika kukubali marekebisho. Na hivyo marekebisho ni lazima yafanyike katika hali ya upendo, upole, unyenyekevu na majadiliano ya kirafiki, isiwe kwa shutuma au ugomvi.

Pamoja na hilo, Papa aliongeza ni lazima majadiliano hayo yafanyike bila kuupoteza ukweli hata kama ukweli huo unamwumiza mtu. Ni lazima kusema ukwelI. Papa alieleza na kuhoji ni mara ngapi wanajumuiya wetu wataeleza ukweli wa mambo ya mtu mwingine, na yale si ya kweli, uzushi, wenye kuharibu sifa ya mtu huyo. Majadiliano - Papa alisema huumiza; na uvumi ni ni kiboko kwa sifa za mtu, ni kichapo kinachoumiza moyo wa mtu. Ni wazi pia kwamba pale wanapoeleza ukweli, si jambo la kufurahisha kusikia, lakini kama maelezo yanatolewa kwa matamshi yenye upendo na urafiki, mtu huweza kukubali alichokifanya hata kama ni tendo la aibu, kwa sababu anafahamu moyoni mwake kwamba ni kweli alifanya hivyo. Hivyo inakuwa tofauti na kusingiziwa. Kwa maana hiyo, ni muhimu kusema ya kasoro za kweli za wengine kwa moyo wa upendo.

Papa aliendelea kueleza kwamba, kurekebishana kidugu ni tendo la uponyaji katika mwili wa Kanisa.Pale inapotokea uwepo wa shimo, katika kiambaza cha Kanisa ni lazima kufanya ukarabati vinginevyo hatimaye ukuta mzima unaweza anguka. Ni kufanya kama akina mama hasa mabibi wazee, wanavyofanya wakati wa kiziba matundu yaliyojitokeza kwenye nguo, huziba tundu hilo polepole, na ndivyo inavyotakiwa katika kurekebishana kidugu. Kama huna uwezo wa kufanya hivyo kwa upendo,ukweli na unyenyekevu, nawe una makosa, una uharibifu ndani ya moyo wako. Huo ni unafiki na upofu ulioatajwa na Yesu, mnafiki, kwanza ondoa pande la ubao katika jicho lako , ndipo uweze kukiona kibazi kidogo katika jicho la nduguyo.

Papa aliasa, maneno haya, yasitutie woga wa kusahihisha wengine iwapo tunaona dhahiri makosa ya wengine , inafaa kuwasaidia kujirekebisha, kwa sababu ni muhimu kusahihishana kwa upendo, ukweli na unyenyekevu.

Na alimalizia homilia na wito wa kumwomba Bwana, daima tuweze kuubeba msalaba mzito kwa ajili ya wema wa kusaidia wengine, tukiw tumejazwa na roho Mtakatifu na upendo, upole na huruma yake. Tuombe ili tusiwe watu wa kuhukumu wengine, bali kusahihishana katika hali ya udugu, upendo, kweli na unyenyekevu katika ukomavu wa kuwa wafuasi wa Kristo. Bwana atusaidia katika huduma hii ya udugu, na uzuri wa kufanya hivyo hata kama inaumiza, ili tuweze kuwasaidia kaka na dada zetu, kuyaisha maisha bora ya utiifu, upendo, ukweli na unyenyekevu.








All the contents on this site are copyrighted ©.