2014-09-09 14:35:42

Kardinali Napier- umuhimu wa Sinodi ijayo juu ya familia


Kardinali Wilfrid Napier, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Durban Afrika Kusini, hivi karibuni amekuwa Rome kuhudhuria vikao mbalimbali vya utendaji katika Idara za Curia. Katika mahojiano na Padre Paul Samasumo wa Redio Vatican, alizungumzia zaidi Familia ya Kikristo, ambayo itakuwa kiini cha majadiliano katika Sinodi maalum ya Maaskofu, itakayofanyika hapa Vatican mwezi ujao, Oktoba 05-19 juu ya mada "Changamoto za Kichungaji kwa familia katika mazingira ya Uinjilishaji".


Kardinali Napier alilenga zaidi katika barua juu ya familia iliyotolewa mwezi Februari na Sekretariat ya maandalizi kwa ajili ya Sinodi, ambamo Papa Franciko ametoa wito kwa Wakatoliki, kuomba kwa ajili ya Sinodi hiyo. Papa ameutaja Mkutano huu wa Sinodi juu ya familia, kuwa ni muhimu na unawahusu watu wote wa Mungu - Maaskofu, Mapadre, Watawa wanaume na wanawake, na wote walio yaweka maisha yao katika uaminifu wa Kanisa duniani kote. Wote wanashiriki katika juhudi hizi za maandalizi kwa ajili ya mkutano huu, kupitia mapendekezo ya utendaji na msaada muhimu wa sala.


Kardinali aliendelea kuirejea barua hiyo ya Papa Francisco pia akionyesha matumaini yake kwamba, itakuwa kweli sinodi maalum ambayo itafuatiwa na Mkutano wa Sinodi ya kawaida ya Maaskofu, mwaka ujao, ambao pia madhari yakeni juu ya familia.

All the contents on this site are copyrighted ©.