2014-09-08 15:30:18

Papa aungana na Maaskofu kutoa wito wa amani Lesotho


Jumapili 7 septemba, baada ya sala ya Malaika wa Bwana, akizungumza na makumi elfu ya mahujaji na wageni, katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Papa Francisko, alitoa wito wa amani kwa mataifa mawili, Lesotho na Ukraine.

Akizungumzia Lesotho, Papa Francisco alisema pia anaongeza sauti yake katika wito wa Maaskofu wa Lesotho, kuomba amani kwa taifa la Lesotho, ana alikemea vitendo vyote vya unyanyasaji na kumwomba Bwana wa amani, arejeshe utulivu katika Ufalme wa Lesotho, amani ambayo ni mizizi wa haki na udugu.

Siku ya Alhamisi, Gazeti la Lesotho Times, lilitaarifu kwamba Baraza la Maaskofu Katoliki Lesotho (LCBC) lilitoa wito wa amani katika mazungumzo kati ya vyama vya upinzani na utawala na pia walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, ihakikishe utulivu katika ufalme huu ambao kuna wasiwasi wa kufumka ghasia.
Wito wa Maaskofu ulitolewa kupitia mkutano wa vyombo vya habari katika mji mkuu, Maseru, Lesotho na Askofu Augustinus Tumaole Bane, Askofu wa Leribe, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu, kwa vyama vya kisiasa na taasisi za kiserikali kama vile vyombo vya usalama, kutatua tofauti zao bila ya kutumia vurugu. Na alisistiza haja ya kuwa na uvumilivu katika utendaji wao. Katika mkutano wa vyombo vya habari, Askofu Bane, alitoa wito huo akiwa na Maaskofu wenzake Askofu Joseph Mopeli Sephamola, Askofu Mkuu Tlali Gerard Lerotholi, Askofu Mkuu Emeritus Bernard Mohlalisi, Askofu Emeritus Sebastian Khoarai, na Askofu John Tlhomola.


Lesotho ni taifa dogo ambalo bado linaheshimu mfumo wa utawala wa kifalme, lina raia milioni 2, na limezungukwa na Afrika Kusini. Lilipewa uhuru kutoka ukoloni wa Uingereza mwaka 1966.

Matatizo ya hivi karibuni Lesotho yalianza, Jumamosi tarehe 30 Agosti, wakati Waziri Mkuu Thomas Thabane alipotoroka na kuvuka mpaka kuingia Afrika Kusini akisema alihofia maisha yake.

Na taarifa za mapema Jumamosi wiki iliyopita zinaeleza, Jeshi la Lesotho , liliteka nyara kituo Kikuu cha Polisi cha ufalme, na kufunga mawasiliano yote ya vituo vya Redio na simu. Na milio kadhaa ya bunduki ilisikika tokea eneo hilo,ghasia zilizosababisha mtu mmoja kupoteza maisha. Katika taarifa iliyotolewa na AFP jeshi limekanusha kuwa na mpango wa mapinduzi ya kijeshi. Na kusisitiza kwamba walio vamia kituo kikuu cha Polisi ni raia mashabiki wa kisiasa waliopata silaha kinyemela.

Waziri Mkuu wa Lesotho Thomas Thabane alirudi Maseru, Ijumaa iliyopita, baada ya Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuingilia kati. Zuma ambaye Mwenye kiti wa SADC, aliitisha mkutano wa dharura Pretoria. Baada ya mkutano kumalizika, SADC ilimtaka Waziri Mkuu Thabane arudi Lesotho. SADC, iliahidi utendaji wa harakakurejesha amani na utulivu Lesotho.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati akitoa ombi lake kwa taifa la Lesotho, pia wakati huohuo kukawa na habari mpya kwamba, mwanajeshi Luteni Jenerali Tlali Kamoli, ambaye alikataa kuachia madaraka kama kamanda wa kijeshi Lesotho, amechukua udhibiti wa ghala kuu la silaha, kwa hisia kwamba, pengine ni maandalizi kwa ajili ya kuanzisha mapambano au hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lakini tamko kutoka jeshi linaonyesha kuwa waminifu bado kwa Naibu Waziri Mkuu, Mothetjoa Metsing, ambaye anayeongoza chama cha Lesotho Congress for Democracy Party, ambaye ni mshirika katika Lesotho serikali ya mseto. Polisi inatuhumiwa kwamba iko karibu sana na Waziri Mkuu Thabane, aliyejiondoa madarakani kwa kutoroka.

Papa Francisko, anatumaini Serikali, wanasisasa na vyombo vya usalama, watasikiliza ombi lake na lile lililotolewa na Maaskofu wa Lesotho, kudumisha amani na majadiliano , kama tu njia inayofaa zaidi, kuondoa kasoro katika utawala, na kujenga haki katika masuala halali na matarajio ya pande zote zinazohusika.
All the contents on this site are copyrighted ©.