Baba Mtakatifu Francisko, amepeleka salaam zake za rambirambi kwa familia za Masista
watatu wanashirika la Mtakatifu Xavery, waliouawa katika nyumba yao ya Kamenge, Kaskazini
mwa mji wa Bujumbura siku ya Jumapili. Majina ya Marehemu Masista ni Sista Olga Raschietti,
Sista Luchia Pulici na Sr Bernadetta Boggian. Wote wanatajwa kuwa raia wa Italia.
Rambirambi za Papa zimetumwa kwa Mjumbe wake wa Kitume nchini Burundi, Askofu
Mkuu Evariste Ngoyagoye na nyingine kwa Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Mtakatifu
Xavery, akionyesha kusikitishwa sana na kilichotokea kwa Masista hao. Papa anatumaini
damu hii ya watu wa Mungu iliyomwangika bure, itaweza kuwa mbegu ya matumaini katika
ujenzi wa udugu wa kweli kati ya jamii ya watu wa Burundi. Na ameahidi kuwakumbuka
katika sala zake mashahidi hawa wa Injili , na ukaribu wake kwa shirika, na jumuiya
ya waamini nchini Burundi.
Mkuu wa Shirika la Watawa Xaverian nchini Burundi,
Padre Mario Pulcini, akithibitisha uwepo wa tukio, ameonyesha hisia kwamba ni tukio
la wizi. Na kwamba, Sista Lucia na Sista Olga, waliuawa Jumapili mchana wakati Sista
Bernadetta, alikwenda kupokea Masista wengine waliowasili katika uwanja wa ndege tokea
Italia.
Wakati aliporejea nyumbani alikutana na hali ya ukimya uliompa wasiwasi
na baadaye akiwa na Padre Mario waliona wenzao tayari walikuwa wameuawa ndani ya nyumba
yao. Na Sista Bernadetta ameuawa usiku wa kuamkia Jumatatu akiwa katika chumba chake.
Askofu Henry, Jimbo la Parma Italia, kwa niaba ya Kanisa lote la Parma, amepeleka
pia niaba ya waamini wa Parma , salaam zake za rambirambi kwa Usharika wa Missionari
Xaverians, wakiwafariji kwa sala ya imani kwa Bwana wa Maisha. Askofu pia ametoa
ombi kwa Wakristo wa Jimbo la Parma na kwa wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka Masista
hawa katika sala zao.