Tumsifu Yesu Kristo! Kwa mara nyingine tena karibu katika makala yetu pendevu tuendelee
kuhekimishana, na hasa kwa kipindi hiki ambapo tunaitazama familia kama shule ya fadhila
na maadili kwa ujumla wake. Nyakati zote, Kanisa linatoa wito kwa wazazi na wote wanaoshika
dhamana ya malezi ya watoto kuhakikisha kwamba watoto wanapatiwa malezi stahiki. Hilo
ni katika kuchangia kumuunda mtu mwenye kufaa katika jamii ya watu. Kwa nafasi
hii mpendwa msikilizaji, tunakualika tutafakari juu ya fadhila ya uaminifu. Maandiko
matakatifu yanausifu uaminifu na mtu mwaminifu anajazwa baraka tele. Mzaburi anatuambia
“Mtumishi mwaminifu atasitawi kama mtende, atasitawi vema kama mwerezi wa Lebanoni”
anaendelea kusema, “waliopandwa katika nyumba ya Bwana watasitawi katika nyua za Mungu
wetu, watajaa utomvu na ubichi, na kuzaa matunda hadi wakati wa uzee” (rej. Zab.92:12-15). Uaminifu
ni nini? Twaweza kusema ni vigumu sana kupata tafanusi sahihi ya uaminifu. Kwa vile
ni sanaa inayohusu maisha ya watu, basi tunaweza kuielewa tu katika uwanda wa maisha
ya kawaida. Hivyo twaweza kusema kwamba, uaminifu ni sanaa ya maisha ya unyoofu wa
akili, moyo na matendo ya kila siku. Kwa nini hayo matatu yaunganishwe katika
uaminifu? Kwa maana chanya, sisi wanadamu wenye akili na utashi, ni kwa akili zetu
tunatambua nini tunapaswa kutenda na tunatenda namna gani. Kwa moyo wetu, tunapenda
kile tunachokitenda na wale tunaowatendea. Na katika matendo ya maisha yetu, tunadhihirisha
kile tunachokijua na tunachokipenda. Hivyo, ule unyoofu katika fikra (akili), unyoofu
katika hisia na unyoofu katika matendo ndiyo uaminifu. Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema
kwamba kuushi kiaminifu ni kuishi katika ukweli, kuishi katika uhalisia wenye haki.
Ni kuenenda pasipo kuleta wasiwasi au mashaka. Uaminifu ni moja ya nguzo muhimu sana
za maisha adilifu. Zamani za wazee wetu, watu walinidhamishwa kwa nguvu sana kuuambata
uaminifu kwa sababu waliamini kwa dhati kwamba, uaminifu ni tunu bora kwa maisha ya
amani na furaha; uaminifu ni msingi wa mafanikio na maendeleo binafsi na maendeleo
ya jamii nzima. Na zaidi sana waliamini kwamba uaminifu ni msingi wa mahusiano mema
kati ya jamii ya mwanadamu inayoishi na ulimwengu wa roho. Ndiyo maana tukichunguza
kwa undani jamii zetu mbalimbali, tutakuta kuna aina za viapo vikali ambavyo vilimlazimu
mtu kuwa mwaminifu kwa agano au kwa wajibu, ili tu kuweza kuleta mustakhabali wa maisha
ya watu. Mtu aliapishwa ili aseme na atende katika unyoofu, aishi katika ukweli wa
moyo. Na kuliwekwa adhabu za kisaikolojia na za kimwili ili kumnidhamisha mtu kutunza
uaminifu. Adhabu za kisaikolojia ni pamoja na aina ya vitisho juu ya madhara mabaya
ya kuvunja uaminifu. Adhabu za kimwili ilikuwa ni pamoja na kutengwa na jamii, mapigo
makali au hata kuuawa kwa namna mbalimbali. Hayo yote yalilenga katika kujenga uzito
wa tunu ya uaminifu na kuwafanya wote waiambate. Leo nasi tunahitaji sana fadhila
hii ya uaminifu katika jamii zetu. Kwa sababu ya kupuuzia kwa makusudi tunu za kiroho,
jamii yetu inateseka sana kwa sababu ya watu kukosa uaminifu katika nyanja zote. Tumejitamadunisha
kwa kuishi kijanja-kijanja, huku tulilinda maslahi binafsi zaidi bila kujali mafaa
ya jamii. Kukosa uaminifu inaelekea kuwa ndiyo utaratibu sahihi wa maisha. Tazama
sasa watu wanavyoteseka, jamii inavyoangamia kwa kupuuza tunu ya uaminifu. Katika
makala hii, tunataka tutafakari na tuiambate tunu hii ya uaminifu katika mapana yake.
Sehemu ya kwanza tunataka tuone juu ya uaminifu katika fikra, uaminifu katika maneno
(yaani ukweli), uaminifu katika mahusiano, uaminifu katika kazi: kazi binafsi na kazi
za umma na uaminifu kwa maisha binafsi. Na sehemu ya pili tutaona pia uaminifu kwa
katika mambo ya Kiroho na mambo yamhusuyo Mungu. Kwa ujumla wake tunaona kwamba,
ni kukosa uaminifu ndio kunatufanya tuvunje amri za Mungu, za Kanisa, tukiuke sheria
za kiasili, tupuuze miongozo sahihi ya jamii zetu na hata tukiuke kanuni za kazi na
kanuni za maisha kwa ujumla. Na matokeo ya kukosa uaminifu ni mahangaiko na mateso.
Tukitaka tuwe salama, na tujibidishe katika uaminifu. Na uaminifu huo ujengwe katika
mioyo ya watu kuanzia katika familia zetu, mashuleni na kila moja wetu aendelee kujilea
katika uaminifu. Sehemu kubwa ya kushindwa kwetu, kuteseka kwa familia ya mwanadamu,
uharibifu wa mazingira ni kwa sababu tu ya kukosa uaminifu. Katika kipindi kijacho
tutaendelea kuchambua uaminifu katika nyanja mbalimbali. Kutoka katika Studio za Radio
Vaticani, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB