Hatua zahitajika kulinda makundi madogo ya Wakristo Iraki
Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kwa mara ingine, imehimizwa na uongozi wa Kanisa la Ulimwengu,
kuharakisha utendaji thabiti utakaoweza kukomesha mara moja mateso na ukatili unaofanywa
na Waislamu wasiovumilia wengine Kaskazini mwa Iraki. Wito huo ulirudiwa kutolewa
siku ya Alhamisi, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kukutana na Kardinali Antonio
Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya kazi za Kichungaji kwa Wahamiaji
na wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Majadiliano yao, yalilenga katika
mahangaiko ya Wakristo wa Iraki na hatima ya vurugu na mauaji yanayoendeshwa na wapiganaji
wababe wa Kiislamu wasiokuwa na uvumilivu kwa watu wasio Waislamu kwa lengo la
kujadili hatma ya Wakristo wanaokimbia vurugu, mauaji na unyama unaofanywa na wapiganaji
wa kiislamu wanajihad nchini Iraki. Taarifa zinaonyesha maeneo mengi nchini Syria
na Iraki, ambao kwa sasa yako chini ya udhibiti wa Kiisalamu, kuna kampeini za kigaidi,
hasa dhidi ya makundi madogo ya watu wasiokuwa waislamu wakiwemo Wakristo. Kardinali
Vegliò akizungumza na Redio Vatican, baada ya kukutana na Papa, alisema kwamba,
Papa amesema, Kanisa lazima liwe mstari wa mbele katika jitihada za kutetea wadhaifu,
kwa kutoa msaada kwa wanaohitaji zaidi, maana haki zao zinagandamizwa. "Kanisa ni
kwa ajili ya maskini na ni sauti ya wanaogandamizwa. Ni lazima lishiriki na kutochoka
kutetea haki, kupitia mahubiri na hotuba; na kushawishi kama inawezekana, hali ya
kisiasa. " Kardinali vegliò aliendelea kusema kwa kurejea maneno ya Papa Francisko,
aliyotoa wakati akirejea toka Korea, kwamba, ni halali kutafuta njia za kusitisha
uchokozi na madhulumu. Lakini akasisitiza, umuhimu wa kutahimini kwanza njia inayofaa
zaidi. Na kwamba ni juu ya jumuiya ya kimataifa kufanya tathmini hii, na kuonya hakuna
kisingizio au udhuru kutofanya hivyo. Na kwamba, vinginevyo hatakuwa na tofauti na
kile kilichofanywa wakati jeshi la Hitler lililofanya mauaji ya kinyama kwa Wayahudi,
na baadaye wengi wakasema, hatukujua kama kulikuwa na unyama mbaya namna hiyo. Huo
ni unafiki. Hivyo kwa wakati huu dunia imekwisha tangaziwa unyama unaofanyika Iraki
na Syria, hakuna kiongozi wa taifa atakayeweza kusema hajui hilo. Hivyo ni wakati
wa mshikamano wa Kimataifa kusitisha unyama huo sasa. Kardinali Vegliò alieleza
na kulaumu jumuiya ya Kimataifa, kwamba mpaka sasa imefanya juhudi kidogo mno, na
hasa viongozi wa Umoja wa Mataifa na Ulaya, ambayo ni kijiografia wako karibu na kanda
hii inayoteswa na vita. Aliongeza, "Kwa bahati mbaya, Ulaya tuna matatizo mengi,
na hasa kutokana na kumezwa na moyo wa ubinafsi na tunajifikiria na kujijali sisi
wenyewe tu , na kupuuza yanayowatokea wengine. "Hata hivyo, matatizo yetu ni kidogo
ikilinganishwa na yale yanayotokea Iraq, watu wanaokimbia ili kuepuka kuchinjwa kama
mbuzi..” Kardinali anatumaini Ulaya sasa itaonyesha kuguswa na madhulumu yanayofanyika
na kuchukua hatua zinazostahili kukomesha unyama huo, kama baadhi ya nchi tayari zimeanza
kufanya hivyo, walau kwa kuwapokea wakimbizi katika nchi yao kama Ujerumani, Ufaransa,
Uingereza, Italia, Hispania, ambayo ni mataifa tajiri ikilinganishwa na wanakotoka
wakimbizi. Na kwamba Kanisa pia limekuwa mshiriki katika kutoa jibu hili. Na aliweka
bayana kwamba, inaposemwa Kanisa si tu kufikiria Vatican au idara "Curia", lakini
ni juhudi za Kanisa zima kila mahali. Amesema Kanisa linaitikia vyema katika utoaji
wa msaada kwa watu hawa maskini, wahamiaji na wakimbizi, waliokimbia makazi yao, kwa
hofu ya maisha yao kukatizwa.