Imani yetu na iwe kioo kinachoonyesha Kanisa Moja na Takatifu
Baba Mtakatifu Francisco, kama kawaida ya mapema siku ya Jumatano alitoa katekesi
yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika Vatican. Mafundisho yake, yalizama
katika kuelezea nini maana ya kukiri “ninasadiki katika Kanisa Moja na Takatifu “.
Papa alianza, .....Ndugu zangu wapendwa, tunakiri katika sala ya Kanisa,
Ninasadiki katika Kanisa moja na Takatifu, kwa sababu asili yake ni katika Utatu
Mtakatifu wa Mungu, fumbo la umoja na ushirika kamili. Ni Takatifu kwa sababu limejengwa
juu ya Yesu Kristo, na kuhuishwa na Roho wake Mtakatifu, na kujazwa juu yake na upendo
wake na wokovu wake. Lakini wakati huohuo ndani mwake mna wadhambi ambao kila siku
huanguka katika udhaifu wa dhambi.
Kwa hiyo imani hii tunayokiri, kama waamini
wa Kanisa Moja Takatifu , inatusukuma katika kuwa waongofu na ujasiri wa kuishi
kila siku katika umoja na utakatifu unaotoka kwa Mungu mwenyewe. Na Yesu Kristo ndiye
msingi wetu wa umoja na utakatifu, na hivyo kama sisi kama hatuko katika umoja na
kama hatuko watakatifu, basi hatuna imani kwake. Lakini pamoja na udhaifu huo bado
hajatuacha peke yetu.
Papa alieleza kuitenga hotuba yake katika vipengere
vitatu, akianza na faraja itokayo kwa Mungu kwamba, waamini hupata faraja kutoka
kwa Yesu, kwa kuwa tangu mwanzo wa kulijenga kanisa lake aliomba kwa Baba yake, Baba
wote wawe na umoja kama wewe Baba ulivyo ndani yangu nami ndani yako, hao nao wawe
ndani yetu ,ili ulimwengu upate kusadiki kwamba wewe ndiwe uliyenituma(Yn17; 11.21-23)
Papa alieleza na kuongeza kwa njisi gani ilivyo vyema kufahamu kwamba Bwana alitupenda
hadi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya sisi wenye dhambi, ili tupate mastahili ya
kuwa katika umoja huu Mtakatifu. Maneno hayo ya Yesu yanatupa utambuzi kwamba kupitia
kwa Yesu pia sisi tunaweza kuingia katika umoja kamili na upendo wake, na katika roho
wake , jumuiya za Kristo zinapata dhamana hii kutambuliwa kama jumuiya ya Kikristo
zilizo jengwa katika utakatifu.
Papa aliomba umoja wa wafuasi wa Yesu, uliosimikwa
zaidi ya yote katika sala ya majitoleo ya mateso na kifo chake msalabani. Kwa ajili
hiyo , Papa alitoa mwaliko kwa watu wote kuendelea kutafakari maneno hayo yaliyo andikwa
katika Injili ya Yohana 11:21-23 akilitaja kuwa ni neno la ujasiri lililotoka kwa
Mungu linalo tuita kila siku katika wogofu. Kupitia kwa Yesu Kristo, ambaye husali
kwa ajili yetu na hasa kwa mateso yake,sis wabatizwa kama kanisa lake sote tuungane
katika umoja nae na Baba na kati yetu.
Baba Mtakatifu aliendelea kueleza kwa
masikitiko kwamba, kwa bahati mbaya , pamoja na kutambua vyema , dhambi ni kinyume
cha umoja, wivu na chuki na ubinafsi kuwa kinyume cha usharika, bado tunakaribisha
ndani ya roho zetu na katika jumuiya zetu na parokia zetu dhambi hizi badala ya kukumbatia
Mapenzi ya Mungu, yanayo tutaka tukuze moyo wa kupendana , kukaribishana na kumpenda
kila mtu kama Yesu anavyotupenda sote. Huo ndio utakatifu wa Kanisa , kutambua sura
ya Mungu katika mwingine . Hivyo,tunapokiri imani hii katika sala ya Nasadiki, tunahimizwa
kujali uongofu wetu , kwa kuwa na ujasiri wa kuishi katika umoja na utakatifu kila
siku, kwa utambuzi kwamba unatoka kwa Mungu. Na kwamba, Yesu Kristo, Neno wa Mungu
aliyemwilishwa na kuja kukaa kati yetu ni chanzo cha umoja wetu na utakatifu, na
kama sisi si wamoja , kama sisi si watu wa Mungu, ni kwa sababu sisi si wafuasi wake.
Hata hivyo, Yesu hatutelekezi, bado yu kado akisubiri tumkaribishe tena mioyoni mwetu.
Kamwe hawi mbali na kanisa lake.
Na Yesu alitolea sala yake kutoka moyoni
kwa Baba yake , akiomba umoja, sisi tunaweza pia sisi kuwa na umoja kati yetu. Na
hivyo kwa maneno hayo, Yesu alitenda kama wakili wetu kwa Baba, ili sisi pia tuweze
kuingia katika ushirika kamili wa upendo pamoja naye; wakati huo huo, anatoa dhamana
kwetu ya kuwa mashahidi wake wa kiroho, na kwa ajili ya utoaji wa majibu mazuri zaidi
kwa mtu yeyote ambaye anaye uliza habari ya wokovu na matumaini yetu (cf. 1 Pt 3
, 15).
Papa aliendelea na kipengere cha pili akirejea Injili ya Yohane 17:21:
wote wawe kitu kimoja, kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yenu, inaweza
wao pia wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma. Papa alifafanua
Kanisa tangu mwanzo ndivyo lilivyojengwa katika umoja kama yalivyokuwa mapenzi ya
Yesu. Na kwamba, Matendo ya Mitume hukumbusha kwamba Wakristo wa kwanza walijulikana
kweli kuwa na "moyo huo wa umoja na roho moja" (Matendo 4 , 32); kisha Mtume Paulo
aliwahimiza wasishau kuwa "mwili mmoja" (1 Kor 12:13).
Lakini uzoefu wa maisha
unatuonyesha kwamba, kuna dhambi nyingi dhidi ya umoja. Na si tu kufikiri juu ya
uzushi mkubwa na ukana Mungu, lakini pia tunapaswa kufikiria juu ya mapungufu madogomadogo
ambayo tunaweza kuyaita ya kawaida yanayotokea katika jumuiya zetu na hata parokia
zetu ambamo washarika wake wameigiwa na dhambi na kusababisha migawanyiko na utengano,
inayoletea na dhambi ya wivu, chuki, fitina n.k. Papa anasema, sawa kibindamu tunaona
kama ni kawaida lakini si Kikristo! Hii hutokea hasa wakati tukiuweka ubinafsi katika
matarajio na ufanikishaji wa malengo ya pamoja. Wengi wetu tunawahukumu wengine
vibaya kwa sababu mimi ninataka kufanikisha lililo ndani mwangu kwa kumwangusha mwingine
kwa nia mbaya. Wengi tunaangalia makosa ya wengine zaidi yetu tukiyafumbia macho badala
ya kutazama ujuzi wao. Mtu anajenga moyo wa kujiona bora zaidi na hivyo kujitenga
na mengine na huo ndiyo mwanzo wa migawanyiko inayotokea hata ndani ya jumuiya za
kanisa, ambazo zinapaswa kuwa mahali pa kuwaungunisha watu na kuw ana roho moja miongoni
wao.
Papa alimalizia na kipengere cha tatu ambamo amezungumzia umuhimu wa
kuchunguza dhamiri akisema kwamba, katika jumuiya ya Kikristo, utengano ni moja ya
dhambi kubwa zaidi, kwa sababu jumuiya ya Kikristo inapaswa kuwa ishara ya kazi ya
Mungu,na si kazi ya shetani. Utengano huharibu mahusiano, na ni mwanzo wa uharibifu
kwa jumuiya na chukizo kwa Mungu. Kumbe Jumuiya au parokia vinapaswa kuwa mahali
pa kukua uwezo wa kusalimiana yetu, kusamehe na kupendana, kwa kuangalia zaidi na
zaidi, ni mahali pa ushirika na upendo. Na hiyo ndiyo maana ya kusali: Nasadiki katika
Kanisa Moja na Takatifu. Hii ni kulitambua Kanisa kuwa mfano wa Mungu, lililojazwa
huruma yake na neema yake.
Papa alikamilisha mafundisho haya kwa kutoa mwaliko
kwa waamini wote , kufanya tafakari ndani ya mioyo yao maneno ya Yesu: "Heri wenye
kuleta amani, maana wataitwa wana wa Mungu" (Mt 5,9). Kwa moyo wa dhati, ni kuomba
msamaha kwa nyakati zote tunapokuwa na matukio ya kuleta mgawanyiko au kutokuelewana
ndani ya jamii zetu, licha ya kuwa na ufahamu kwamba, mgawanyiko huvunja umoja na
ushirika katika jumuiya na wala hatuwezi kuendelea kutembea katika njia ya uongofu
ulio imara.Na hivyo tumwombe Mungu, ili kwamba mahusiano yetu ya kila siku yaweze
kuwa zaidi mazuri na furaha na yenye kutoa mwangwi mzuri katika uhusiano kati yetu
na kati yetu a Yesu na katu yetu na Mungu Baba.