Hakika Kristu ni Mwana wa Mungu wa walio Hai, sote tukiri hivyo ....Papa
Kanisa ni watu wanaotembea na Mungu katika maisha yao ya kila siku wakiwa wamejawa
na imani, upendo na matumaini kwa Mungu Baba. Ni jumuiya ya watu iliyoanzishwa na
Yesu Mwana wa Mungu, ambayo hupata nguvu zake kutoka juu, na kuwa imara, mwamba wa
imani isiyovunjika. Ni hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Jumapili wakati
wa sala ya Malaika wa Bwana, aliyosali pamoja na maelfu ya mahujaji na wageni, waliokusayika
katika uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.
Papa alieleza juu ya uhusiano
wa waamini na Yesu kwamba, hujenga Kanisa. Na kwamba Yesu tangu mwanzo, alifikiri
kuijenga jumuiya iliyo imara yaani Kanisa, mfano wa jengo imara. Na ndivyo alivyo
mwita SimonI kati ya mitume wake kumi na wawili na kumpa jina jipya Petro, ambalo
katika lugha ya kiebrania, lina maana ya mwamba. Katika Biblia neno hili mwamba,
ni rejea kwa Mungu. Na SimonI alichaguliwa na Yesu, kuitwa Mwamba, (Petro) si kwamba
alikuwa na sifa za kipekee za kibinadamu, lakini alikuwa na imani ya kweli thabiti
kwa Yesu, imani iliyotoka juu.
Yesu alisikia moyoni mwake furaha kuu, kwa
sababu alitambua Simoni, kwa neema ya Baba na Roho Mtakatifu, amepewa imani ya
kumainika, ambamo, Yeye Yesu, ataweza kulijenga Kanisa lake, jumuiya ya waaamini
wote wanaobatizwa katika Jina la Kristo. Yesu kwa upendo wake mkuu aliyatoa maisha
yake kwa ajili ya Kanisa, watu waliosimikwa katika imani asilia thabiti , yenye kujenga
uhusiano thabiti nae, uhusiano katika upendo, usharika na matumaini. Na haya ni mahusiano
yanayopaswa kuwepo kati yetu sisi na Yesu kama Kanisa lake. Yesu anapenda kuliona
kanisa lake alilo lianzishwa, linaendelea kutembea katika mwanga wa imani imara na
matumaini thabiti katika njia yake.
Baba Mtakatifu alieleza na kusema , Ndugu
zangu wapenzi, kile kilichotokea kwa Mtakatifu Petro , ni tukio na hoja kwa kila Mkristo,
kuona ukomavu wake katika kumwamini Yesu Mwana wa Mungu aliye Hai . Na hivyo Somo
la Injili ya Matayo 16;13-20, ni changmoto kwetu sote kujiuliza, kwa namna gani tunatembea
katika njia hii ya imani kwa uaminifu? Kila mmoja analo jibu moyoni mwake. Baba Mtakatifu
alieleza, Yesu anapenda kukaa katika moyo wenye imani ya kweli , aminifu na thabiti
kama mwamba. Na yeye huyaona mawe yaliyo hai yanayo ijenga jumuiya yake , jumuiya
iliyosimikwa kwa Kristo , jiwe kuu la pembeni.
Papa pia alizumgumzia upande
wa Petro kwamba, kwa imani yake, alipewa dhamana ya kuwa mwamba wa Kanisa ambamo
kanisa linajengwa juu yake, na hivyo kunatakiwa kuonekana umoja wa waamini wote kama
kanisa moja lililojengwa juu ya mwamba huu, Petro. Somo hili ni mwaliko kwa kila mbatizwa,
kutafakari msimamo wa imani yake , kwa sababu katika usharika wa imani, iwezekane
leo hii kuendelea kujenga Kanisa lake moja Takatifu la Mitume, katika kila kona ya
dunia, lililosimikwa katika mwamba imara.
Baba Mtakatifu alibaini kwamba
, hata leo hii kuna watu wengi wanaofikiri kwamba Yesu alikuwa nabii mkuu na mwalimu
wa hekima na mfano wa haki , lakini Yesu hata leo hii anawauliza wanafunzi wake, ambao
ni sisi wabatizwa wote, je ninyi mwasema mimi ni nani? Papa alitoa mwaliko kwa wote
kufikiri sana juu ya hilo. Kabla ya kutoa jibu, zaidi ya yote ni kumwomba Mungu Baba
, kupitia kwa Mama Bikia Maria tupate neema ya zawadi ya kutoa jibu la kweli kutoka
ndni ya mioyo yetu kukiri kwamba, Wewe ni Kristo , Mwana wa Mungu wa Walio Hai. Kuikiri
imani kama tunavyosali katika sala ya kweli ya Nasadiki. Papa alikamilisha kwa kuwataka
wote waliokuwa wakimsikiliza kurudia mara tatu maneno : Wewe ni Kristo , Mwana wa
Mungu wa walio hai.