2014-08-22 12:00:28

Papa Francisko yuko mbioni kutoa waraka wake mpya juu ya mazingira na ekolojia


Jumatatu , Baba Mtakatifu akikutana na wanahabari akiwa ndani ya ndege kutokea Korea Kusini, alithibitisha kwamba, tayari ameandika waraka wake juu ya mazingira na uko katika hatua za mwishomwisho . Na kwamba ameuandika waraka huo kwa kushirikiana na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Haki na Amani, na watalaam wengine.

Ingawa Papa hakutaja lini waraka huo utatoka lakini alisema, waraka huu utakuwa mrefu zaidi ya waraka juu ya Furaha ya Injili kwa kuwa anajaribu kutoa majibu ya maswali mengi magumu na tatanishi. Na kwamba, inawezekana kujadili uwakili wa viumbe na mazingira kwa uwazi lakini ni tu kwa kiwango fulani, na kisha nadharia za kisayansi huingilia kati baadhi wakiwa ni wapembuzi yakinifu, na wengine kwa hisi tu.

Norman Levesque, Mkurugenzi wa Mradi wa Kanisa wa Shirikisho la Kiekumeni la Canada Montreal, alisema anatarajia waraka wa Papa Francisko utakuwa umefuata mawazo endelevu juu ya mazingira na maendeleo kama walivyofanya watangulizi wake, Papa Paulo VI ambaye alilenga zaidi maendeleo endelevu, Papa Yohana Paulo II alizama zaidi katika haki za kijamii na Papa Benedikto xvi, alilenga katika heshima na utaratibu wa uumbaji. Na hivyo anatumaini Kanisa litaendelea kutembea kwa makini katika njia za maendeleo katika muktadha wa haki za ekolojia, utaratibu wa viumbe na heshima yake.

Levesque alionyesha matumaini yake kwamba, utume wa kanisa katika huduma ya kutunza mazingira , utaweza kutoa majibu katika kipeo cha mazingira, kwa kusoma yaliyo andikwa katika Biblia , simulizi za Watakatifu , sala ya Kiekaristi , fadhila na rejea zake zote.









All the contents on this site are copyrighted ©.