2014-08-22 09:57:59

Mara baada ya kutembelea Iraki Kardinali akutana na Papa


Kardinali Fernando Filoni, wiki iliyopita aliyekwenda Iraki kama Mjumbe wa Papa, Jumatano ya wiki hii, alirejea Roma na kukutana na Papa. Kardinali kwa muda wa wiki zima alikuwa Iraki , kuonyesha mshikamano wa dhati wa Papa Francisco kwa raia wanaoteswa na hasa Wakristo wa Iraki, wanaoishi hali ngumu kutokana na imani yao. Kardinali Filoni, katika muda huu wa wiki moja alitembelea sehemu mbalimbali zinazo toa hifadhi kwa watu waliokimbia ghasia, fujo na mashambulizi yenye mauaji yanayofanywa na vikundi vya Kiislamu vinavyojiita wanajihad, ambao wanalazimisha watu kuongokea Uislamu, katika nyanda za Nanawi, Kaskazini mwa Iraki.

Kardinali Filoni, akizungumza katika mahojiano na Sergio Centofanti wa Redio Vatican baada ya kukutana na Papa siku ya Jumatano ameeleza kwamba, mkutano wake na Papa Francisco mara tu baada ya kurudi kwake Roma, limekuwa ni jambo jema, na inaonyesha jinsi Papa anavyojali watu wateswa Mashariki ya kati , na hivyo Papa alipenda kujua mara moja hali halisi zinazoendelea Iraki. Na hivyo alimweleza Papa hali halisi zilivyo, hasa katika maeneo aliyotembelea yanayo kaliwa na Wakristo wengi kama eneo la Yazidis, ambako alikuwa makini sana. Na alieleza juu ya uhuru wote, matarajio ya Wakristo, na wasiwasi wa viongozi wa kanisa katika eneo hilo.

Na Papa alionesha kukuguswa kwa namna ya kipekee na maelezo hayo, hasa katika mtazamo wa haja ya kuandaa mipango ya kidharura inayoweza kuwapatia makazi ya kufaa, watu waliokimbia nyumba zao na sasa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi zaidi , mahali popote, uwanjani, vyumbani, ukumbini, na kila nafasi waliyoweza kuipata katika eneo walikodhani walau kuna usalama zaidi. Na licha ya kukimbia ukatili wa wanajihadi pia kulikuwa na joto kali ikifikia degree 47-48, na pia kuna ukosefu wa vitu mhimu kama maji hata ya kunawa tu , ukosefu wa kivuli, hata kidogo, na mambo mengine muhimu ni dharura za kipekee zinazohitaji msaada wa haraka kusaidia watu hawa hasa watoto, wazee, wagonjwa. Hayo ni mambo misingi ya kwanza kufikiriwa, na ndipo ifuatie nini cha kufanyika kurejesha amani na utulivu kwa watu hawa.
Kardinali Filoni anasema, huo ndiyo ukweli alioona katika ziara yake Iraki, na bila shaka, Wakristo wana hamu ya kurejea katika makazi yao , wanatamani kurudi katika vijiji vyao. Na hivyo wanaililia jumuiya ya kimataifa iwawezeshe kurudi makwao na kuanza maisha mapya ya kawaida. Bahati mbaya tukio la wiki hii la unyama uliofanywa kwa Mwandishi wa habari wa Marekani kuchichwa kama kuku, watu wametiwa hofu mpya ya kurudi majumbani mwao. Watu hawana tena hiyo haraka ya kutaka kurudi majumbani mwao. Hivyo kunahitajika tena muda kidogo wa kupata uhakika zaidi katika usalama wa watu hao. Na alionyesha matumaini yake kwamba, ni kuvuta saburi kidogo katika jambo hili.


Kardinali ametaja nia na asili ya ziara yake kwamba ilikuwa katika misingi ya ubinadamu. Na kwa heshima ameifanya ziara hii kwa moyo na upendo mkuu, kuona hasa ni yapi yanahitajika kupewa kipaumbele katika utoaji wa msaada kwa watu, na kuona kwamba kwamba wanahitaji, faraja na matumaini na kutiwa moyo katika tumaini la upendo wa Kristo. Na kwamba kwake yeye pia umekuwa ni wakati nzuri sana kiroho, kwa sababu kuwa karibu na watu wateswa kama ndugu, husaidia si tu kuona matatizo, lakini pia kutazama hali za siku za baadaye, na kisha kushirikiana nao. Na kwamba, ameguswa sana na upendo, ukarimu, na tabasamu za watoto wengi, pamoja na wema wa watu wengi na wanawake, aliokutana na kuzungumza nao na kuwabariki. Kardinali anatumaini watu hawa wataweza tena kurejea makwao na kuishi kwa amani na utulivu wa kudumu.







All the contents on this site are copyrighted ©.