2014-08-22 09:33:56

Bikira Maria Malkia wa huduma kwa Mungu na binadamu!


Mama Kanisa tarehe 22 Agosti, anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu, Sherehe ambayo ilitangazwa na Baba Mtakatifu Pio XII kunako mwaka 1954 mara baada ya kuhitimisha Maadhimisho ya Mwaka wa Bikira Maria. Katika tukio hili, Baba Mtakatifu Pio XII alisema kwamba, Bikira Maria ni Malkia, heshima ya hali ya juu kabisa inayoinua moyo wake na kama kielelezo makini cha zawadi na karama alizojaliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni Mama ambaye anaendelea kuwashirikisha binadamu wote hazina kubwa inayobubujika kutoka katika upendo wake wa Kimama.

Baada ya mageuzi ya Liturujia yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican Siku kuu hii kwa sasa inaadhimishwa siku nane mara baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, ambayo imesherehekewa hapo tarehe 15 Agosti.

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Bikira Maria asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili baada ya kumaliza mwendo wa maisha yake hapa duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni: mwili na roho, akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa Ulimwengu ili afananishwe kikamilifu zaidi na Mwanaye aliye Bwana wa mabwana; mshindi wa dhambi na mauti. (Reje. LG 59.)

Hiki ndicho kiini cha Kumbu kumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, kwani anafananishwa zaidi na Mwanaye mpendwa katika hija ya maisha hapa duniani, utukufu mbinguni ambayo Yesu anaonesha kwamba Yeye ni njia, wokovu na matumaini ya waja wake.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto akitafakari kuhusu kumbu kumbu hii anasema kwamba, Bikira Maria ni Malkia wa mbingu kama matokeo ya muungano wake wa dhati na Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo; uwepo wake mbinguni, yaani kwa kuungana na Mwenyezi Mungu. Bikira Maria anashiriki ile dhamana ya Mwenyezi Mungu kwa ulimwengu kwa kuwashirikisha walimwengu upendo wa Mungu, Ikumbukwe kwamba, Yesu ni Mfalme ambaye ufalme wake unajionesha katika huduma, upendo; kwa kupenda, kusaidia na kuhudumia.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anasema, Siku ile ya Alhamisi kuu, alionesha unyenyekevu wa hali ya juu, alipowaosha mitume wake miguu, tofauti kabisa na wakuu wa ulimwengu huu. Yesu ni Mfalme anayehudumia wafanyakazi zake, kielele cha utume na maisha yake hapa duniani.

Haya pia yanaweza kusemwa juu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu; ni Malkia kwa ajili ya huduma kwa Mungu na mwanadamu. Ni Malkia anayemwilisha ile zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya Ukombozi wa mwanadamu. NI Malkia anayewasaidia watu kwa kuwapenda kwani anatambua mahitaji yao msingi, ni mama na mtumishi mnyenyekevu!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedito XVI anabainisha kwamba, Bikira Maria kuitwa Malkia ni kielelezo cha imani, furaha mapendo, anaendelea kuwasaidia waamini wanapomkimbilia katika shida na magumu ya maisha. Ikumbukwe kwamba, Ibada kwa Bikira Maria ni jambo msingi sana katika maisha ya kiroho. Waamini wajenge utamaduni wa kumkimbilia Bikira Maria katika sala zao, wakionesha imani na matumaini. Bikira Maria ni Malkia, yuko mbele ya Mwenyezi Mungu; ni Mama ambaye yuko karibu na wote wanaoteseka na kulalamika huku bondeni kwenye machozi.







All the contents on this site are copyrighted ©.