Kardinali Lluis Martinez Sistach, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcellona, Hispania
anasema kwamba, Waraka wa Injili ya Furaha, Evangelii gaudium uliotolewa na Baba Mtakatifu
Francisko ni muhimu sana katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji mpya na dhamana
ya waamini walei kuyatakatifuza malimwengu.
Hapa Yesu
Kristo anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kujenga mazingira yatakayowawezesha
watu kukutana na Yesu, ili kumwinua tena mwanadamu aliyeanguka na kuelemewa na madhaifu
yake. Umefika wakati wa kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa Mataifa, changamoto
inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Miji inahitaji uwepo wa malaika wengi zaidi
kuliko kujazwa na hofu za mashetani.
Mashetani wanaozungumzwa hapa ni ukosefu
wa fursa za ajira, uchafuzi wa mazingira, umaskini wa hali na kipato, ukosefu wa makazi
bora ya watu, mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema, watu kutoaminiana,
ubinafsi, uchoyo, wizi na ufisadi, vita, nyanyaso, madhulumu na hofu!
Malaika
wanaoendelea kuboresha maisha ya watu mijini ni pamoja na: familia, mahali ambapo
watu katika raha na mahangaiko yao ya ndani wanapata kitulizo. Katika miji ile ambayo
idadi ya Wakatoliki inazidi kupungua mwaka hadi mwaka, hapa ni kumwilisha Injili ya
Furaha kadiri ya changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kujikita
katika ushuhuda wa maisha, kama chachu ya utakatifu, kiasi hata cha kujisadaka kama
alivyofanya Askofu Oscar Romero. Wakristo katika miji mikubwa wanaweza kuwa ni malaika
walinzi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.
Mikakati ya kichungaji katika
miji mikubwa iwalenge na kuwashirikisha vijana ambao kwa sasa wengi wao wanaogelea
katika mitandao ya kijamii, huko huko watangaziwe Injili ya Furaha na waelekezwe namna
ya kukutana na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kanisa
liendelee kujielekeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kujikita katika upendo,
umoja na mshikamano wa kidugu unaoongozwa kanuni auni.
Waamini walei kwa njia
ya ushuhuda wa maisha yao, wawe makini kueneza Injili ya Furaha kwa kuwashirikisha
wengine ile furaha ya kukutana na Yesu. Licha ya kazi kubwa iliyofanywa na Mitume
wa Yesu katika Kuinjilisha, lakini wanawake wa Kanisa la mwanzo kwa njia ya ushuhuda
na tunu zao za kimama walikuwa mstari wa mbele katika mchakato wa Uinjilishaji, changamoto
hata leo hii kwa Wanawake Wakatoliki kuhakikisha kuwa wanajifunga kibwebwe kuwaonjesha
jirani zao ile furaha ya Injili, kwa njia ya ushuhuda na karama mbali mbali walizokirimiwa
na Roho Mtakatifu.
Kanisa Katoliki katika miji mikuu liwe makini kusoma alama
za nyakati anasema Kardinali Sistachi kwa kutambua fursa, matatizo na changamoto zilizopo,
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Yesu Kristo ambaye ni chemchemi ya Uinjilishaji,
kazi inayoendelezwa na Roho Mtakatifu.
Padre Jean Bosco Matand Bulembat, mkuu
wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kinshasa na bingwa wa Maandiko Matakatifu anasema, Yesu
alikuwa na uhusiano mkubwa na miji ya nyakati zake alitembelea na kuhubiri: Nazareti,
Capernaumu, lakini zaidi mjini Yerusalemu, kote huku Yesu alikuwa anamtafuta mwanadamu,
ili kumwinua katika utu na heshima yake; kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu bila
ubaguzi. Kwa njia hii, Yesu alitambulikana na wengi kuwa ni Mwinjilishaji nambari
moja!
Alionesha ujasiri na moyo wa kukutana na kila mtu, hii ndiyo changamoto
kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa liwe na ujasiri wa kuwatangazia
wafanyakazi na wakulima Injili ya Furaha, kwa kuwashirikisha wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Dhamana hii itekelezwe na waamini walei ambao kwa njia ya unabii, ukuhani
na ufalme wao, wasaidie kuyachachua malimwengu kwa harufu ya utakatifu wa maisha.
Watu waonjeshwe upendo wa Mungu unaokoa na kuponya; watu watangaziwe Kweli
za Kiinjili bila shuruti bali kwa kugusa katika uhuru wa mtu binafsi; waamini wawaonjeshe
jirani zao upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; washiriki katika
raha na majonzi ya jirani zao.
Ikumbukwe kwamba, Kanisa lina dhamana ya Kuinjilisha,
kumbe, Makleri wasikae wala kucheza mbali katika mcakato huu kwa umakini wa Neno la
Mungu na ushuhuda wa maisha yao ya Kikuhani yenye mvuto na mashiko kwa watu! Kila
siku kuna watu wapya wanaingia mijini, hawa wapokelewe na kushirikishwa maisha na
utume wa Kanisa, hakuna mgeni wala “Mnyamahanga, Kyasaka wala mtu wa kuja”, wote ni
wa Kristo!
Changamoto nyingine ni huruma na upendo wa kimama unaopaswa kuoneshwa
na Kanisa, kwa kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ushuhuda
na utakatifu wa maisha ni chachu ya Uinjilishaji mjini, watu wamechoka kusikia porojo,
wanataka kuona imani katika matendo!
Imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.