2014-08-21 08:46:39

Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, maadhimisho ya Sinodi maalum ya maaskofu kwa ajili ya familia kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba, 2014 yanapania kuangalia kwa umakini mkubwa kuhusu familia ambayo kimsingi ni urithi wa binadamu. RealAudioMP3

Haya ni mambo msingi ambayo yanafafanuliwa kwenye Hati ya kutendea kazi ya Sinodi ya Maaskofu, kama inavyojulikana kwa lugha ya kitaalam, Instrumentum Laboris. Mababa wa Sinodi wataangalia mwanga na giza linaloiandama familia bila kushinikizwa na mwelekeo wa vyombo vya habari ambavyo wakati mwingine vina ajenda iliyofichika. Dhamana na wajibu wa Mababa wa Sinodi ni mkubwa mbele yao na kwamba, Kanisa na hata dini mbali mbali zina matumaini makubwa katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya maaskofu kwa ajili ya familia.

Mababa wa Sinodi anasema Kardinali Baldisseri watachambua tema zote zilizowasilishwa kwenye Hati ya kutendea kazi baada ya kupata majibu yaliyotolewa kwenye maswali dodoso thelathini na nane yaliyotumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali duniani na taasisi zenye dhamana ya maisha na utume wa familia. Dhamana ya Familia imebainishwa kwa kina na mapana katika hati hii ya kutendea kazi ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu yenye vipengele mia moja hamsini na tisa.

Tema zote hizi zimeshibana sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia yanayojikita katika msingi wa Injili na imani ya Kikristo kwa kuendelea kusoma alama za nyakati na kwamba, hapa hakuna utamaduni unaoweza kujidai kwamba, unakumbatia kwa dhati kabisa imani ya Kikristo, ndiyo maana bado kuna haja ya Kanisa kuendelea Kuinjilisha na Kutamadunisha, ili imani ya Kikristo iweze kuota mizizi katika maisha na vipaumbele vya Wakristo na hatimaye, kumwilisha imani hii katika matendo.

Kutokana na mwelekeo huu mpana, Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anataka kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai, ili kujibu kwa ufasaha fursa, changamoto na matatizo yanayozikabili familia sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Baldisseri anasema Kanisa litaendelea kuwa aminifu kwa mafundisho yake tanzu, kanuni maadili na sheria za Kanisa.

Mababa wa Sinodi watakuwa na fursa ya kushirikisha: uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa Injili ya familia katika maeneo husika, kwa kusukumwa na ukweli, uwazi, ujasiri, uhuru na ujasiri wa kuweza kuibua mbinu mkakati wa maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Baldisseri anakumbusha kwamba, Hati ya kutendea kazi ni mwongozo unaopania kuwasaidia Mababa wa Sinodi katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia na wala si Waraka wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Huu ni muhtasari wa takwimu, maelezo, mapendekezo, uzoefu, ukweli na mang’amuzi ya maisha ya familia katika mwanga na giza lake.

Maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia kunako mwaka 2015, yatakuwa na dhamana kubwa zaidi ya kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu, ili aweze kuyafanyia kazi na kutoa mwelekeo wa utume na maisha ya familia ndani ya Kanisa Katoliki. Huu ni mchakato wa hija ya maisha ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo bila kuacha mambo ambayo ni kweli, haki na msingi katika maisha na utume wa familia, ili kutangaza Injili ya Familia inayojikita katika taalimungu na nidhamu.

Ikumbukwe kwamba, familia ni chombo cha majadiliano ya kiekumene na kidini. Hapa kuna ndoa za mseto kati ya Wakristo na waamini wa dini mbali mbali; familia na sheria asilia, familia na usawa wa kijinsia ni kati ya mambo ambayo yanaweza kujadiliwa na waamini wa dini mbali mbali, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Ndoa za watu wa jinsia moja ni changamoto kubwa ya kimaadili, utu wema na ustawi wa familia.

Hiki ni kielelezo cha kupukutika kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema anasema Kardinali Baldisseri. Uchunmba sugu na baadhi ya vijana kutokuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuogopa athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni changamoto kubwa katika kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Majibu yaliyotolewa kwenye maswali dodoso yanaonesha kwamba, watu wengi wanathamini familia na umuhimu wa mahusiano yake na Kanisa pamoja na Jamii katika ujumla wake licha ya changamoto na kinzani zinazoweza kujitokeza. Watu wengi wameshuhudia umuhimu wa maisha ya ndoa na familia kama njia ya kutangaza Injili ya Familia kwa watu wa kizazi hiki wanaoonekana kukengeuka na kutopea katika malimwengu. Familia ya Kikristo ni mfano bora wa kuigwa na familia nyingine duniani. Matatizo na changamoto zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha watu kumezwa na malimwengu, dalili za ukanimungu, vita, majanga asilia, uhamiaji, ujinga, umaskini na maradhi.

Mambo yote haya yanaacha madonda makubwa kwa wanafamilia wengi, Mama Kanisa kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, anaalikwa kuwaganga wote hawa kwa kuwatangazia Injili ya Familia, uzuri wa upendo pasi na kujibakiza; umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, malezi na majiundo makini katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia itakayoibuliwa na Mababa wa Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya familia anasema Kardinali Baldisseri inapania pamoja na mambo mengine, kumwilisha kwa kina na mapana Mafundisho na nidhamu ya Kanisa kama inavyojidhihirisha katika Sakramenti, Neno la Mungu na maisha ya Wakristo. Waamini wote wanahamasishwa kuwa ni watangazaji wa Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa imani katika matendo.

Hapa anahitimisha Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano na Gazeti la L’Osservatore Romano kwa kusema kwamba, Katekesi makini ni muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia. Watu wafundishwe, waelimishwe na waelewe mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuyatolea ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.