2014-08-21 12:21:00

Mhariri wa Radio Bakhita aachiliwa huru, lakini kituo bado kimefungwa!


Uongozi wa Kituo cha Radio Bakhita inayomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini, Jumatatu tarehe 18 Agosti 2014 umeomba radhi kwa vyombo vya usalama vya Serikali ya Sudan ya Kusini na kuwaomba kumwachilia huru Mhariri wake aliyekamatwa na kuwekwa kizuizini.

Bwana Albino Tokwaro amewaambia waandishi wa habari kwamba, walisimulia mkasa mzima na viongozi wa vyombo vya usalama wa taifa wakamua kuwasamehe, kwani walitangaza habari kwamba vikosi vya serikali vilikuwa vimewavamia na kuwashambulia wanajeshi wa upinzani, habari ambayo haikuwa na ukweli!

Wananchi wa Sudan ya Kusini wanaendelea kujifunza kutekeleza demokrasia na kwamba, waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini na sahihi kwa habari wanazochapisha na kutangaza, kwani zinaweza kusababisha mtafaruku katika jamii kama ilivyotokea kwa vyombo vya usalama. Waandishi wa habari wawe na uhakika wa vyanzo vyao vya habari!

Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES linasema kwamba, Mhariri wa Radio Bakhita ameachiliwa huru, lakini Kituo cha Radio bado kimefungwa, ili kusubiri maelekezo kutoka kwenye vyombo vya usalama wa taifa jinsi ambavyo Radio hii itapaswa kuendesha shughuli zake kwa siku za usoni.

Lengo ni kutaka kupunguza programu za kisiasa, jambo ambalo kwa sasa linajadiliwa baina ya viongozi wa pande hizi mbili. Muswada wa sheria ya vyombo vya habari Sudan ya Kusini uliopitishwa na Bunge, bado haujatiwa mkwaju na Rais Salva Kiir, ili uanze kutekelezwa rasmi!.







All the contents on this site are copyrighted ©.