Inasikitisha kuona watu wanajitosa mhanga ili kusababisha vifo kwa wengine!
Askofu mkuu Alfred Adewale Martins wa Jimbo kuu la Lagos, Nigeria anasema kwamba,
anasikitishwa na taarifa zinazotolewa kuonesha kwamba, Kikundi cha Kigaidi cha Boko
Haram sasa kinaanza kuteka na kumiliki maeneo ya nchi, kiasi hata cha kulifanya Jeshi
la Serikali ya Nigeria kuwa na wakati mgumu wa kuweza kuyakomboa tena maeneo haya
yanayokaliwa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram.
Askofu mkuu Martins anayasema
haya kutokana na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kuteka vijiji kadhaa Kaskazini
mwa Nigeria na kuanza kuvitawala kwa mabavu pamoja na mfululizo wa milipuko ya mabomu
ya kujitoa mhanga yanayoendelea kuhatarisha maisha na mali za wananchi wa Nigeria.
Inasikitisha kuona kwamba, watu wanajitoa mhanga kwa kile wanachodhani kwamba, hii
ni vita ya kidini.
Askofu mkuu Martins anaendelea kuwatia shime wananchi wa
Nigeria kutokatishwa tamaa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi
cha Boko Haram pamoja na wasi wasi wa kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, ambao
kwa sasa unaendelea kuwa ni tishio la usalama na maisha ya watu Afrika Magharibi.
Hadi sasa Cameroon imefunga mipaka yake na nchi jirani kama sehemu ya mikakati
inayopania kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo. Cameroon imekuwa ikitoa
hifadhi kwa makundi makubwa ya watu wanaokimbia mashambulizi ya kigaidi kutoka nchini
Nigeria, kumbe kufungwa kwa mipaka ya Cameroon kuna madhara makubwa hata kwa wakimbizi
kutoka Nigeria.