Epukeni kishawishi cha kuuza ubora wa elimu ili kupata kura za watanzania!
Shule Katoliki ni rasilimali ya thamani kubwa katika mchakato wa ujenzi wa upendo,
umoja na mshikamano; ni mahali pa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu
na kitamaduni. Vijana warithishwe elimu inayosheheni: ukweli, wema, amani na upatanisho
wa kijamii, ili vijana waweze kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo katika hija
yao ya maisha.
Askofu Severine
Niwemuguzi, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum
na Radio Vatican anabainisha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linajizatiti
kuhakikisha kwamba, linatoa elimu bora ambayo kimsingi ina gharama zake. Hii ni changamoto
kubwa kwa shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kujikuta kwamba, zinatoza
ada ya kiwango cha juu, kiasi cha kuwafanya watoto wa maskini kushindwa kupata elimu
bora inayotolewa na Kanisa, ikizingatiwa kwamba, hawa ni walengwa wa kwanza.
Hadi
sasa hakuna jibu la mkato kuhusiana na changamoto hii, lakini Familia ya Mungu nchini
Tanzania inaendelea kutafakari jinsi ya kuziwezesha hata Familia maskini kupata fursa
za elimu zinazotolewa na Kanisa.
Askofu Niwemugizi anasema kwamba, miongozo,
sera na mifumo inayotolewa na Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwachanganya wadau wa
elimu hasa kuhusiana na viwango vya ufaulu wa mitihani ambao umegubikwa kwa kiasi
kikubwa na mambo ya kisiasa badala ya kujielekeza katika taaluma ya elimu.
Kutokana
na sera kama hizi, Kanisa linajikuta linakabiliwa na changamoto ya utoaji wa elimu
bora na kwamba, kuna haja ya sauti ya kinabii kusikika kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa
katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya watanzania katika sekta ya elimu. Tanzania
haina budi kushinda kishawishi cha kuuza ubora wa elimu kwa kutafuta kura za watanzania!
Kuna haja ya kuwa na sera na miongozo ya kudumu, ili kuhakikisha kwamba, maboresho
yanayokusudiwa katika sekta ya elimu yanazaa matunda muafaka na kwamba, wanafunzi
wanaohitimu masomo yao nchini Tanzania wanaweza kukabiliana na ushindani kutoka sehemu
mbali mbali za dunia.
Madhara ya kushuka kwa viwango cha ubora wa elimu nchini
Tanzania yamejionesha hivi karibuni kwani ufaulu wa wanafunzi wanaopaswa kujiunga
navyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania umeshuka sana na hivyo kuwa
na idadi ndogo ya wanafunzi wanaopaswa kujiunga na elimu ya juu. Hizi ni changamoto
za kibinadamu na kisiasa zaidi zinazokamisha mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu
nchini Tanzania.