Elimu ni ufunguo wa mageuzi ya kijamii nchini Madagascar
Kanisa Katoliki nchini Madagascar, limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma
za kijamii hasa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu, kama sehemu ya
mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kanisa linapenda
kuweka uwiano bora kati ya akili, tamaduni na kanuni maadili ili kuwasaidia wananchi
wa Madagascar kupambana kikamilifu na changamoto za maisha. Ni changamoto iliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar wakati walipofanya
hija ya kitume mjini Vatican hivi karibuni.
Madagascar imebahatika kuwa na
rasilimali nyingi ambazo kama zingeweza kutumika barabara, leo hii watu wake wangekuwa
wamecharuka kwa maendeleo, lakini kwa bahati mbaya, wananchi wengi bado wanaendelea
kuogelea katika dimbwi la umaskini, magonjwa na njaa. Kinzani za kisiasa, kijamii
na kiuchumi zimepelekea watu wengi kukosa matumaini ya kesho iliyo bora zaidi anasema
Askofu Rosario Vella wa Jimbo Katoliki la Ambanja, lililoko Kaskazini mwa Madagascar.
Elimu makini ni njia pekee inayoweza kuwajengea uwezo wananchi wa Madascar
kuweza kupambana na changamoto za maisha na hatimaye, kujipatia maisha bora zaidi.
Kuna umati mkubwa wa watoto wadogo ambao wanapaswa kuwa darasani, lakini hawana nafasi
hii, kiasi kwamba, kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika nchini Madagascar
kimefikia asilimia 31% ya wananchi wote wa Madagascar, hali ambayo inatisha na kuhuzunisha.
Hii inaonesha kwamba, jitihada za Umoja wa Mataifa kupambana na baa la ujinga
kama sehemu ya mikakati ya utekelezaji wa Maendeleo ya Millenia zinakabiliwa na changamoto
kubwa! Kiwango na ubora wa elimu inayotolewa nchini Madagascar ni cha hali ya chini
kabisa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, walimu wanaofundisha shuleni wana kiwango
cha chini cha elimu.
Kanisa Katoliki limejipambanua kwa kuwaaandaa walimu
kitaaluma na kimaadili ili waweze kutekeleza vyema wajibu wao ndani ya jamii na matokeo
yake ni kwamba, shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zinaonesha mafanikio
makubwa katika sekta ya elimu. Wanafunzi wanaosoma katika shule na taasisi za elimu
za Kanisa Katoliki licha ya kupatiwa ujuzi na maarifa, wanafundishwa pia misingi ya
nidhamu, umuhimu wa familia, mshikamano na upendo wa kidugu na kwamba, utu na heshima
ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.
Haya ni mambo ambayo pia
yamo katika maisha, mila na desturi njema za wananchi wa Madagascar, lakini kwa sasa
yanaonekana kutoweka kama ndoto ya mchana! Kanisa Katoliki limeendelea kutoa huduma
katika sekta ya afya kwa wote bila ubaguzi.
Tangu kuteuliwa kwake kuwa Askofu
wa Jimbo Katoliki la Ambanja kunako mwaka 2007, Askofu Vella alisoma alama za nyakati
na kutambua kwamba, ujinga ndilo lililokuwa tatizo kubwa kwa waamini wake, kiasi kwamba,
tangu wakati huo, akajielekeza kwa kuwekeza katika sekta ya elimu na leo hii amekwishajenga
shule za msingi 50 zilizoenea vijijini.
Vijana wamemchangamotisha kujielekeza
katika ujenzi wa Chuo kikuu na tayari Chuo kikuu cha Jimbo Katoliki la Ambanja kimezinduliwa
mwaka 2014. Hapa vijana wamecharuka katika masomo kwani wanatambua kwamba, elimu ni
ufunguo wa maisha kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kitivo cha sheria kinaonekana
kuwa na mvuto kwa wanafunzi wengi, ili kuimarisha utawala wa sheria na haki nchini
humo, kwani mwelekeo wa sasa ni mwenye nguvu mpishe, vinginevyo utakiona cha mtema
kuni!
Wananchi wa Madagascar wana imani na matumaini makubwa na Kanisa, kwani
Kanisa limekuwa nao bega kwa bega wakati wa raha na shida, wakati wa kuomboleza na
kucheka! Kanisa litaendelea kujielekeza katika kutafuta, kulinda na kutetea mafao
ya wengi nchini Madagascar anasema Askofu Rosario Vella wa Jimbo Katoliki la Ambanja,
Madagascar.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.