Sinodi za majimbo nchini Burundi zinapania kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja
wa kitaifa, ili kukoleza imani, matumaini na mapendo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi limejiwekea mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji
kwa kuadhimisha Sinodi za Majimbo ili kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja na mshikamano
wa kitaifa pamoja na kukoleza imani, matumaini na mapendo kati ya watu. Hayo yamesemwa
hivi karibuni na Askofu Gervais Banshimiyubusa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Burundi.
Kwa njia ya
maadhimisho ya Sinodi za Majimbo, Maaskofu wanapania kuona kwamba, waamini wanaifahamu
imani wanayoiungama katika Kanuni ya Imani, Imani wanayoiadhimisha katika Sakramenti
na Liturujia ya Kanisa; Imani wanayoimwilisha katika matendo adili, wakiongozwa na
Amri za Mungu na Imani wanayoisali na kuitekeleza kwa vitendo katika matendo ya huruma.
Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika
mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Burundi linasema, kati ya zawadi kubwa waliyopewa na Roho Mtakatifu
katika siku za hivi karibuni ni kukamilika kwa tafsiri ya Biblia Takatifu kwa lugha
ya Kirundi, ambayo ni lugha ya taifa nchini humo. Biblia hii itawasaidia waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kuweza kusoma, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno
la Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Kanisa Katoliki nchini Burundi
linaendelea kukua na kupanuka, kwani hivi karibuni kumeanzishwa Seminari kuu na hivyo
kulifanya Kanisa Katoliki Burundi kuwa na Seminari kuu nne, dalili za kuongeza kwa
miito ya Upadre na Utawa. Kwa sasa Maaskofu wanapenda kujielekeza zaidi katika majiundo
makini ya Majandokasisi: kiakili, kiutu, kiroho na katika shughuli za kichungaji,
ili Mapadre wanaotoka Seminarini humo waweze kuwa wamefundwa na kuiva barabara tayari
kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.
Maaskofu wanaishukuru Familia
ya Mungu nchini Burundi ambayo inaendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza
malimwengu. Hili pia ni jambo la kumshukuru Mungu!
Baba Mtakatifu Francisko
alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu katoliki Burundi wakati wa hija yao
ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano aliwataka kujielekeza kwa
namna ya pekee katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Burundi. Alimkumbuka
kwa namna ya pekee Marehemu Askofu mkuu Michael A. Courtney aliyekuwa Balozi wa Vatican
nchini Burundi aliyeuwawa kikatili na watu wasiojulikana kunako tarehe 29 Desemba
2003. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, mwaminifu
kwa Kristo na Kanisa lake katika utekelezaji wa utume wake nchini Burundi.
Baba
Mtakatifu Francisko aliwapongeza Maaskofu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo
makini ya vijana wa kizazi kipya ili waweze kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa
Burundi inayojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa!