2014-08-19 09:40:55

Siku ya ubinadamu duniani!


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 19 Agosti 2014 inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu, ili kuwakumbuka wafanyakazi 22 wa Umoja wa Mataifa waliouwawa kwa kulipuliwa na bomu kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad, kunako tarehe 19 Agosti 2013.

Matukio ya wafanyakazi kutoka Umoja wa Mataifa kutekwa nyara, kujeruhiwa vibaya na hata kupoteza maisha yao yanazidi kuongezeka siku hadi siku. Hawa ni watu wanaojitosa mhanga kwa ajili ya huduma kwa watu wanaohitaji msaada zaidi. Kumbe, siku hii ni kwa ajili ya kusherehekea ari na moyo wa watu kujisadaka kwa ajili ya jirani zao!

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa 132 wametekwa nyara; wafanyakazi 155 wameuwawa kikatili na wengine wanaendelea kuchungulia kaburi huko Sudan ya Kusini na Ukanda wa Ghaza.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake kwa Siku hii anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwaenzi wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliotekwa nyara, waliojeruhiwa au kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza dhamana yao kwa kuwalinda wafanyakazi walioko kwenye eneo la tukio kwa wakati huu. Ni mwaliko wa kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watu sehemu mbali mbali za dunia.

Watu wanapaswa kutambua kwamba, kuna mamillioni ya watu yanayotegemea maisha na ustawi wao kutokana na huduma zinazotolewa na wafanyakazi hawa. Kumbe, mashambulizi dhidi yao ni kudhohofisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuwahudumia walengwa, kiasi cha kuwaacha wakiwa wamekata tamaa pamoja na kuhatarisha maisha yao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, majanga ya kimataifa yameongezeka maradufu na kwamba, hali hii inatarajiwa kuongezeka zaidi. Haya ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu, mipango mibovu ya miji, makundi makubwa ya wahamiaji, ukosefu wa usalama wa chakula na maji pamoja na kuongezeka kwa majanga asilia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada wa kimataifa, kumbe Umoja wa Mataifa unaendelea kuwategemea watu wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine. Hawa ni watu wanaotaka kuleta mabadiliko katika sura ya nchi. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha juhudi za watu hawa, inasherehekea mshikamano wa kimataifa unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine!







All the contents on this site are copyrighted ©.