Serikali ya Sudan ya Kusini kutokana na kile inachodai kuwa ni sababu za usalama wa
taifa, imeamua kuifungia Radio Bakhita inayomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo kuu la
Juba, kutorusha matangazo yake. Baadhi ya wanafanyakazi katika kituo hiki wametiwa
mbaroni.
Radio Bhakita ilifungwa tarehe 15 Agosti 2014 baada ya kutokea kinzani
kati ya Serikali na Chama cha Upinzani. Vituo kadhaa ya Radio nchini Sudan ya Kusini,
vimefungiwa au vimepata shinikizo kutoka katika vikosi vya ulinzi na usalama kiasi
kwamba, kwa sasa au vimesitisha huduma kwa muda au vinasua sua katika utekelezaji
wa dhamana yake.
Mkataba wa amani ili kusitisha vita na machafuko ya kijamii
na kisiasa bado haujatekelezwa na pande zinazohusika. Umoja wa Mataifa unasema, kwa
sasa inaonekana kwamba, biashara haramu ya silaha inazidi kupamba moto Sudan ya Kusini,
hali ambayo itasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!