Jaji mstaafu Lewis Makame amefariki dunia Jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, National Electoral Commission
(NEC) kufuatia taarifa za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume hiyo, Jaji
Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame kilichotokea katika Hospitali ya AMI Trauma Centre
Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Agosti, 2014.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Mwenyekiti wa Kwanza
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Mheshimiwa
Lewis Makame ambaye amelitumikia Taifa letu katika Utumishi wa Umma kwa uaminifu,
uadilifu, bidii na umahiri mkubwa”,amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu
zake.
Katika utumishi wake, Marehemu Jaji Lewis Makame, enzi za uhai wake,
alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa na
baadaye Mwenyekiti wa NEC ambayo aliiongoza kwa miaka 17 mfululizo hadi alipostaafu
mwaka 2011. Uongozi wake ulichangia sana kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano
wa kitaifa katika mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
“Ni
kwa kutambua kipaji kikubwa cha uongozi alichokuwa nacho Marehemu Jaji Lewis Makame,
Taifa letu limepoteza mtu muhimu sana kwani hata baada ya kustaafu kwake alikuwa bado
anahitajika sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika mambo mengi yanayohusu
maendeleo ya nchi yetu”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,
“Kutokana na msiba
huu mkubwa, nakutumia Salamu za rambirambi kwa kumpoteza aliyekuwa Kiongozi Mahiri
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kupitia kwako, naomba Salamu zangu za rambirambi na
pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti.
Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho
ya Marehemu, Jaji Lewis Makame, Amina”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.
Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu
mkubwa, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awape moyo wa uvumilivu, ujasiri
na subira Wanafamilia wote, ndugu na jamaa wa Marehemu, ili waweze kuhimili machungu
ya kuondokewa na Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mwenyezi Mungu.