Zingatieni: taaluma, weledi, maadili na sheria za kazi!
Askofu Antony Crowley, Makamu mwenyekiti wa Tume ya Elimu, Baraza la Maaskofu Katoliki
Kenya amewataka wakuu wa shule kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu
wao kwa kuonesha uongozi bora unaojidhihirisha kwa kuwafahamu vyema wanafunzi wao
pamoja na kuzingatia: taaluma, weledi na kanuni maadili na sheria za kazi.
Askofu
Crowley, ameyasema haya hivi karibuni alipokuwa anazungumza na wakuu wa shule zinazomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Kenya pamoja na wadau wengine katika sekta
ya elimu. Wakuu wa shule wanapaswa kuwa ni kielelezo bora cha nidhamu, utendaji bora
wa kazi kwa kutekeleza wajibu wao unaozingatia utu na heshima ya binadamu.
Umoja
na mshikamano eneo la kazi ni mambo msingi katika maboresho ya sekta ya elimu. Walimu
wajitahidi kuwafahamu wanafunzi wao barabara ili kuona mambo yanayokwamisha maendeleo
yao kitaaluma na kutafuta mbinu za kuweza kupambana na vikwazo kama hivi. Wanafunzi
waheshimiwe na kuthaminiwa, wapewe miongozo na malezi sahihi katika maisha yao, ili
mwisho wa siku waweze kuwa ni raia wema.
Wakuu wa shule katika mkutano huu
wamezindua pia Umoja wa Wakuu wa Shule za Kikatoliki, kwa ufupi CaSPA, kazi iliyofanywa
na Askofu Maurice Muhatia Makumba, Mwenyekiti wa Tume ya elimu na mafundisho ya dini
shuleni kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.