Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Karibu kwa mara nyingine tena katika kipindi chetu pendevu. Kwa sasa tunazitembelea
fadhila mbalimbali zenye kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku.
Tunajifunza
fadhila hizi ili sisi wenyewe tujiunde hivi tuwe watu tunaopokeleka na kufikika katika
maisha yetu ya kila siku. Ni imani yetu kwamba, ni jukumu la kila mmoja kuchangia
katika hali njema ya jumuia tunamoishi. Kwa lile kanisa la nyumbani ambalo kimsingi
ni shule ya maadili na fadhila, tusikose kuwafundisha watoto wetu fadhila hizi. Huko
ndiko wanakoanza kuundwa katika utu wema.
Kwa siku ya leo tutazame ukweli kama
fadhila. Ukweli ni nini? Ni uwiano kati ya kinachosemwa, hali halisi na hukumu ya
akili. Kwa mfano kama kinachosemwa ni mtu, katika uhalisia awe ni mtu na akili ihukumu
kuwa kweli huyu ni mtu. Tunapotazama ukweli kama fadhila kwa siku hii ya leo, tunataka
tujinidhamishe katika kupenda kusema ukweli daima.
Nyakati zetu hizi, kumezuka
na kukua sana utamaduni wa kusema uwongo, yaani kuficha ukweli. Watu tunasema uwongo
mwingi sana hata usio na tija yoyote. Kutokana na kutokuwa wakweli mdomoni mara nyingi,
tumekwisha kuziathiri na akili zetu nazo, hazipendi tena kufikiri ukweli. Kuna wanaosema
kwamba matumizi ya simu za mkononi nyakati zetu yamechangia sana kujengeka kwa tabia
ya uongo. Ukweli wa hilo sina uhakika. Simu huwa haisemi uwongo, ni mtumiaji ndiyo
husema uongo.
Mtume Paulo anatuonya akisema “basi uvueni uwongo, kila mmoja
anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo”
(Ef. 4:25). Maandiko matakatifu yanatuasa daima tuseme ukweli, uwongo ni tabia ya
kishetani. Shetani ndiyo baba wa uongo, na vitoto vyake vyote vina tabia ya baba yao.
Maanake uongo unatushetanisha, tunafanana na shetani. Yoshua bin Sira anasema “kataa
kabisa kusema uongo, maana uongo hauleti jema lolote (7:13), maana kama vile aibu
imjiavyo mwizi ndivyo hukumu kali itakavyompata mdanganyifu” (5:14).
Tena
Yoshua Bin Sira anaendelea kutuonya juu ya ubaya wa uongo akisema “uongo ni doa baya
sana kwa mtu; uko daima mdomoni mwa mpumbavu. Afadhali mwizi kuliko mwenye tabia ya
uongo. Lakini wote wawili wataangamia. Tabia ya kusema uongo huleta fedheha, nayo
itabaki daima na mwenye kusema uongo” (YbS.20:24-26).
Kama kawaida yetu, rai
tunaipeleka katika Kanisa la nyumbani, yaani familia. Wazazi na wote wenye dhamana
ya malezi, tuwafundishe na tuwajenge watoto wetu katika roho ya kupenda kusema ukweli.
Ni bahati mbaya pale ambapo watoto wetu hujifunza kusema uongo kutoka kwetu sisi watu
wazima. Familia ya watu waongo huwa haifilisiki fujo. Baba mwongo, daima anamdanganya
mama, mama naye mwongo daima anamdanganya baba, watoto nao lazima watafundishwa kusema
uongo ili kulinda uovu wa wazazi. Wazazi waliozoea kudanganyana, lazima watawafundisha
watoto kusema uwongo. Ukweli ukitoweka, kila kitu kinakuwa na wasiwasi.
Walimu
pia huko mashuleni, wawanidhamishe watoto kusema ukweli daima. Pasipo kujenga akili
katika kuheshimu na kupenda kusema ukweli, tunajenga jamii ya waongo. Na uongo ukitawala
katika kila kona ya utendaji, hapo ufanisi hautapatika na hatutafikia malengo, kwa
vile waongo na wasingiziaji wenye kujitetea kwingi kwa sababu za uongo. Kukosekana
kwa ukweli wa maneno na ukweli wa mambo, husababisha mateso katika jamii.
Mtu
asiyependa ukweli, mwenye kububujika maneno ya uwongo daima, huwa anaharibu utulivu
wa watu waishio kwa amani. Mzaburi anataja ukweli kama mmoja ya sifa za mtu anayestahili
kukaa katika hema ya Bwana. Anauliza na kujibu “Bwana ni nani atakaye kaa hemani mwako?...ni
mtu atendaye daima yaliyo mema, asemaye ukweli kutoka moyoni” (rej. Zab. 15:1-2).
Mpendwa
msikilizaji, na tujinidhamishe katika kusema ukweli. Uongo unachukiza sana. Na mtu
akizoea kusema uongo, atausema tu kila wakati hata bila sababu. Ukweli humpa mtu heshima,
uongo humletea mtu fedheha na dharau. Ukweli hutupatia uhuru na usalama. Na Kristo
alisema “ukweli utawapeni uhuru”. Mpendwa msikilizaji, fanya kama zoezi la kiroho,
anza polepole kujizoeza kusema ukweli. Siku nzima ipite bila kusema uwongo, kisha
wiki zima, kisha mwezi mzima, na baadaye itakuwa fadhila ya kudumu, kuenenda bila
kusema uwongo. Tunakutakia zoezi jema!
Kutoka katika Studio za Radio Vaticani,
ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.