2014-08-17 08:46:03

Ushuhuda na majadiliano katika ukweli na uwazi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili asubuhi tarehe 17 Agosti 2014 amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, kwenye madhabahu ya Haemi, ambayo kimsingi ni kumbu kumbu ya Mashahidi waliojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kuna watakatifu wengi ndani ya Kanisa ambao majina yao hajaandikwa kwenye vitabu vya watakatifu, lakini ni kielelezo cha utakatifu wa Kanisa.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi dhamana na utume wa Kanisa Barani Asia, sehemu ambayo ina utajiri mkubwa wa tamaduni na mapokeo; mahali ambapo Kanisa linachangamotishwa kutoa ushuhuda wa Injili kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa wote. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo watambue utambulisho wao na kuutolea ushuhuda makini katika misingi ya ukweli na uwazi, ili yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Wakristo watambue mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea katika hija ya maisha yao na kwamba, kuna mambo ambayo Mwenyezi Mungu anayataka kutoka kwa Wakristo. Ili majadiliano haya yaweze kuwa na mwelekeo wa pande mbili, lazima Wakristo wafungue akili na mioyo, ili kuwakubali na kuwapokea watu wengine pamoja na tamaduni zao. Hapa Baba Mtakatifu anakazia mambo makuu mawili, yaani ushuhuda na majadiliano na kwamba, kuna mambo makuu matatu ambayo yanapaswa kuangaliwa na kuepukwa katika hali ya ukomavu.

Kwanza kabisa anasema Baba Mtakatifu ni mawazo mepesi mepesi yanayowasukuma wengi katika hali ya kuchanganyikiwa na kukata tamaa. Hiki ni kishawishi kikubwa ambacho kinagusa pia Jumuiya za Kikristo, ambazo zinapaswa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye msingi wa maisha yao. Yeye ni alfa na omega, nyakati zote ni zake. Mawazo mepesi mepesi si tu kwamba, yanajitokeza kama dhana bali pia yanamwilishwa katika matendo bila ya wengi kufahamu na hivyo kudhohofisha utambulisho wa aina yoyote ile!

Baba Mtakatifu anasema, jambo la pili linalohatarisha msingi wa utambulisho wa Wakristo ni kufanya mambo kwa juu juu tu bila kuzamisha mizizi hasa katika shughuli za kichungaji, kwani mambo mengi yanafanyika kama mtindo wa maisha, unaovamia na kutoweka mara. Hii ni mikakati ya kichungaji ambayo inavutia machoni pa pa watu kutokana na nadharia zake hasa miongoni mwa vijana.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, vijana wanahitaji katekesi makini na viongozi thabiti katika maisha ya kiroho; kwa kukita mizizi kwa Yesu na katika kweli, vinginevyo maisha ya fadhila yatageuka kuwa kama mchezo wa kuigiza, majadiliano ya dhati yatageuka kuwa ni "mchapo" kwa kukubaliana au kutokubaliana.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kishawishi cha tatu ni usalama unaojificha katika majibu mepesi mepesi, sentesi zilizokwisha kupikwa, sheria na kanuni. Imani kimsingi haijitafuti yenyewe bali ina tabia ya kutoka nje. Ni zawadi inayojieleza kwa watu ili waweze kuifahamu, kiasi hata cha kuweza kuimwilisha na kuitolea ushuhuda katika matendo; imani inaibua utume.

Utambulisho wa Kikristo unajipambanua kwa kuwa na dhamana ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuwapenda jirani; kujisadaka kwa ajili ya huduma, kama kielelezo cha ushuhuda wa kile wanachoamini na yule ambaye wamemwekea matumaini yao. Imani hai kwa Kristo ndio msingi madhubuti wa utambulisho wao wa kina unaozaa matunda yanayokusudiwa. Ni imani inayozaliwa na kurutubishwa na neema ya majadiliano na Kristo katika mwanga wa Roho Mtakatifu, kiasi cha kuzaa haki, wema na amani.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawataka Maaskofu Katoliki Barani Asia kuhakikisha kwamba, utambulisho wao wa Kikristo unajitokeza kwa nguvu kabisa katika proramu za katekesi, mikakati ya kichungaji miongoni mwa vijana na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utambulisho huu ujioneshe katika mchakato wa kuwahamasisha vijana kujiunga na maisha ya Kipadre na Kitawa.

Mwishoni mwa hotuba yake kwa Maaskofu kutoka Barani Asia, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na utambulisho wa Kikristo uliowazi kabisa, kwani majadiliano ya kweli yanahitaji uwezo wa mtu kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kanisa lioneshe uwezo wa kusikiliza si tu maneno yanayozungumzwa na watu, bali liguswe pia uzoefu, matumaini, matarajio, matatizo na mambo msingi ambayo wanayapatia kipaumbele cha pekee.

Tabia hii ya kuguswa na mahangaiko ya wengine iwe ni matunda ya mwelekeo wa maisha ya kiroho na uzoefu wa mtu binafsi unaowawezesha waamini kuwathamini wengine kama ndugu zao, ili kuwasilikiza kwa makini, licha ya maneno na matendo yao, bali kile ambacho wanapenda kuwashirikisha kutoka katika undani wa mioyo yao. Mwelekeo huu wa ukweli na uwazi kwa uwe ni mwongozo hususan Barani Asia ambako Vatican haijafanikiwa kuwa na uhusiano mkalimifu, ili kukuza na kuendeleza majadiliano si tu ya kisiasa bali majadiliano ya kidugu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mara baada ya hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko na msafara wake pamoja na Maaskofu kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia walipata chakula cha mchana.







All the contents on this site are copyrighted ©.