Msifanyie mzaha ugonjwa wa Ebola, toeni ushirikiano!
Kardinali Thèodore Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal anawataka
wananchi pamoja na viongozi wa Serikali nchini humo kuwa makini katika kupambana na
ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa umekuwa ni tishio kubwa la maisha na usalama wa wananchi
kutoka Afrika Magharibi. Ugonjwa huu unaendelea kusababisha mateso na mahangaiko kwa
watu wengi, kiasi kwamba, watu wengi wamechanganyikiwa kutokana na madhara yanayosabishwa
na ugonjwa huu.
Kardinali Sarr amewataka wananchi kutambua ukumbwa wa tatizo
hili na kwamba, watu wengi wameguswa na madhara yake, kumbe hakuna sababu ya watu
kufanya mzaha kuhusu kujikinga na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kuenea kwa ugonjwa
huu ambao umetangazwa kuwa ni janga la kimataifa. Wananchi waoneshe ushirikiano kwa
Wizara ya afya na Serikali pale wanapotambua wagonjwa walioambukizwa virusi hivi katika
maeneo yao, ili hatua madhubuti ziweze kuchakuliwa haraka.
Kardinali Thèodore
Adrien Sarr ameyasema haya wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho, kwenye madhabahu ya Popenguine, Jimbo kuu la Dakar, Senegal.
Amewakumbuka watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita nchini Syria na wale wanaodhulumiwa
na kunyanyaswa kutokana na imani yao Kaskazini mwa Iraq.
Kardinali Sarr amewataka
viongozi wa kidini nchini Senegal kujibidisha katika kufunda dhamiri nyofu, ili wawe
waweze kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kujielekeza
zaidi katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Tofauti mbali
mbali zinazojitokeza katika maisha ya watu ni utajiri mkubwa na kamwe kisiwe ni chanzo
cha vita na maafa kwa watu wasiokuwa na hataia. Hapa kuna haja ya kusimama kidete
kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, ili watu waishi kwa
amani na utulivu wakifurahia maisha yao!