Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na Familia ni chanda na pete!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA linaendelea
kukazia kuhusu Uinjilishaji Mpya kama fursa inayowawezesha waamini kujikita katika
wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani ya Kanisa Katoliki kwa kutoa kipaumbele cha
kwanza kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia na umuhimu wa Jumuiya ndogo ndogo za
Kikristo.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania anasema kwamba, familia ni nguzo msingi katika kurithisha imani, utu na maadili
mema. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu ya pili ambayo inapaswa kuwa ni matunda
ya familia thabiti za Kikristo, ili kuimarisha msingi wa Kanisa mahalia.
AMECEA
imeendelea kukazia uimarishaji wa mikakati ya kichungaji kwa ajili ya Familia pamoja
na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Ujenzi wa Kanisa mahalia hauna budi kuanza katika
familia na baadaye kuimarishwa katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kwani hapa ni
mahali ambapo Wakristo wanakutana kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika
uhalisia wa maisha yao.
Ni mahali pa kuimarisha katika imani, matumaini na
mapendo, tayari kumwilisha imani kwa Kristo na Kanisa lake katika matendo. Jumuiya
ndogo ndogo ni shule ya ukarimu, huruma na mapendo ni mahali pa kuimarishana katika
maisha ya Kisakramenti. Padre Raymond Saba anasema Familia na Jumuiya ndogo ndogo
zilizokomaa ni kielelezo cha uhai wa Kanisa mahalia.