Askofu Gervas Rozario wa Jimbo Katoliki la Rajshahi, huko Bangaladesh anasema kwamba,
matatizo na changamoto mbali mbali zinazoikumba familia ni sehemu ya maisha na utume
wa Kanisa kwani Kanisa linatambua kwamba, Familia ni chombo muhimu sana katika kurithisha
imani, maadili na utu wema ndani ya Jamii na kwamba, ni nguzo msingi ya maisha ya
kijamii.
Katika barua
yake yake ya kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “Utangazaji wa Injili ya Familia
ya Kikristo” anafafanua kwamba, Familia ni muhimu sana katika maisha, ustawi na maendeleo
ya jamii husika kama ilivyo pia hata kwa Mama Kanisa. Kumbe, Kanisa litaendelea kuwekeza
katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, kila familia
ya Kikristo ni Kanisa dogo la nyumbani, linalowajibika kuwa ni moja, takatifu, katoliki
na la mitume, tayari kuwatangazia wengine Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa
maisha.
Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia,
familia inakumbana na umaskini wa hali na kipato, ulevi wa kupindukia, kinzani za
kifamilia, utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini;
ndoa za chapu chapu pasi na msingi kamili wa upendo! Kukua na kuongezeka kwa familia
tenge ambazo nyingi zinahudumiwa na wanawake peke yao kutokana na wazazi wa kiume
kwenda kutafuta riziki mbali na familia zao pamoja na ukosefu wa mbinu makini za mawasiliano
kati ya wanandoa na matokeo yake ni wanandoa kukosa amani na furaha ya ndoa.
Injili
ya Familia ya Kikristo inapenda kukuza na kuimarisha tunu bora za maisha ya ndoa na
familia kwa kuhakikisha kwamba, familia zinatekeleza wajibu wake wa malezi kwa watoto
wao. Hapa Kanisa linapenda kujenga na kukuza sanaa ya mawasiliano kati ya wanandoa,
ili wanapowasiliana basi iwe ni fursa ya kushirikishana upendo unaojielekeza zaidi
katika umoja, majadiliano, msamaha na haki.
Mihimi ya Injili, yaani Mapadre,
Watawa na Makatekista wanahamasishwa kutembelea familia, ili kuzisaidia katika kutambua
wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na kuendeleza majiundo makini
kwa wanandoa watarajiwa ili waweze kufahamiana, kupendana na kuheshimiana. Kwa wale
wambao wanaishi tayari katika maisha ya ndoa na familia wanapaswa kupewa Katekesi
endelevu, ili kung’amua changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha yao, ili kuweza
kuzikabili kwa busara, upendo na ujasiri. Vijana wa kizazi kipya waelimishwe ili
kutambua umuhimu wa maisha ya ndoa na familia, ili wawe tayari kufanya maamuzi magumu
katika maisha yao kwa kuchagua kufunga ndoa ya Kikristo na kufuata masharti yake,
yaani hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Yataka moyo kweli kweli kufunga ndoa ya
Kikristo. Vijana wafahamiane kwanza na wakubaliane kwa kusukumwa na upendo thabiti
na wala si makando kando yake, kama vile pochi! Waswahli wanasema, hapendwi mtu, ila
pochi, lakini kumbe haya ni mambo mpito!
Askofu Gervas Rozario anasema kuna
baadhi ya Wakristo ambao wanaendelea kuishi katika uchumba sugu, hawa pia ni walengwa
katika mikakati ya kichungaji, ili kurekebisha hali yao tayari kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa na wala wasiwe ni watazamaji hasa wakati wa kushiriki
Sakramenti za Kanisa.