2014-08-16 11:39:51

Hali ni tete sana nchini Iraq!


Kardinali Fernando Filoni, Mjumbe wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, Ijumaa tarehe 15 Agosti 2014 ametembelea Jumuiya ya wakimbizi wa Amadya, Zakho na Duhok, ili kuonesha mshikamano wa dhati kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuwasilisha mchango wa Dolla za Kimarekani 25, 000, ili kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Jeshi la Jihadi, Kaskazini mwa Iraq.

Wananchi waliokutana na Kardinali Filoni wameelezea mateso makali wanayokumbana nayo kiasi cha kudhalilisha utu na heshima yao kama binadamu na kwamba, kama Jumuiya, wamejeruhiwa sana kiasi kwamba, jamii imetengana na kusambaratika. Wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kutowasahau katika shida na mahangaiko yao. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kuimarisha mikakati yake ili kusitisha mauaji haya ya kimbari yanayotokana na misimamo mikali ya kiimani na chuki za kidini.

Kardinali Filoni anasema, amefanikiwa kutembelea kambi mbili za wakimbizi na kujionea mwenyewe mateso yao. Jumuiya ya Amadya, Ijumaa tarehe 15 Agosti 2014 imeadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, wakiomba ulinzi na tunza ya Mama wa Mungu na Kanisa. Watu wanateseka, wengi wamepoteza ndugu na jamaa zao; wanakabiliwa na uhaba wa huduma za afya na chakula. Watu wanaendelea kutekwa na kunyanyaswa, haya ni mateso ambayo watu wanapaswa kuyafahamu, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuchukua hatua madhubuti.

Kardinali Filoni, Ijumaa jioni amekutana na viongozi wakuu wa Kanisa na kwa pamoja wameadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni na idadi kubwa ya waamini wameshiriki katika tukio hili muhimu sana katika imani yao. Pamoja na mateso yote haya bado kuna baadhi ya Wakristo wamebaki katika maeneo yao ili kulinda Makanisa yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.