2014-08-15 09:54:21

Vijana na likizo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linawakumbusha vijana na wanafunzi ambao kwa sasa wamemaliza pilika pilika na patashika nguo kuchanika kwa ajili ya mitihani na tayari wanaanza likizo ya kipindi cha kiangazi kuhakikisha kwamba, wanatumia muda huu vyema kwa ajili ya kuku ana kukomaa: kiroho, kimwili na kiutashi wakiwa pamoja na familia zao. RealAudioMP3

Hiki si kipindi cha kujirusha, kwani vijana wengi wamejikuta wakijichumia majanga binafsi, familia na jamii katika ujumla wake kwa kutozingatia utu na maadili mema wakati wa likizo! Hiki ni kipindi cha vishawishi vinavyopaswa kuratibiwa kwa kuwa na utashi thabiti. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malta unawataka wazazi na walezi kuwa karibu na vijana wao nyakati hizi za likizo ili kuwasaidia kukua na kukomaa barabara!

Likizo ni kipindi ambacho kinatoa mwanya kwa vijana kukuza na kuendeleza ut una vipaji vyao, kwa kutumia vyema uhuru binafsi na muda alionao. Ni wakati wa kukuza na kuendeleza mahusiano bora ya kijamii kwa kutambua kwamba, wakati wa shule pengine vijana hawana muda sana wa kukaa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Ni kipindi cha kazi, vijana wajitume kusaidia kazi za nyumbani, kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na familia. Ni kipindi cha vijana kukuza na kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Kwa vijana ambao walikuwa na visingizio vya kukosa muda wa kwenda Kanisa kutokana na kubwana sana na masomo, likizo wajitahidi kushiriki hata katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, si tu wakati ule watakapokuwa wanatafuta cheti ili kuandikisha ndoa au wanapojisikia kuwa na fununu ya wito wa kipadre na maisha ya kitawa! Vijana tangu mwanzo wajifunze utamaduni wa kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kama kielelezo cha imani katika matendo! Maaskofu Katoliki kutoka Malta wanakazia mambo makuu matatu: Kazi, Familia na Mapumziko!

Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linasema, vijana wakati wa likizo wanaweza kusaidia kuchangia gharama za maisha katika familia zao kwa kufanya kazi za muda pale inapowezekana. Hiki ni kipindi cha mpito kutoka shule na kuingia katika ulimwengu wa kazi, vijana wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao, kwa kupewa mshahara wa haki.

Familia ziwe makini kuhakikisha kwamba, vijana hawa wanafanya kazi kadiri ya umri na uwezo wao. Vijana wawe na muda wa kutosha kukaa pamoja na familia zao, hiki kiwe ni kipaumbele cha kwanza kwa vijana wenyewe na wazazi wawe mstari wa kwanza kuonesha mfano na ushuhuda wa maisha.

Likizo ni muda wa vijana kujichotea nguvu ili kupambana kikamilifu na changamoto za maisha. Vijana wajifunze kutumia vizuri muda wao na kwamba, wawe makini ili wajanja wachache wasije wakawatumbukiza katika nyanyaso na dhuluma mbali mbali kwa kigezo cha kutaka kuwapatia fedha, kwani fedha inaweza kuzaa fedhea.

Vijana wajiepushe na makundi ya watu waliokengeuka kimaadilina kiutu kwani wanaweza kujikuta huko huko wanajifunza matumizi haramu ya dawa za kulevya na ukahaba.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linawaalika vijana kujitahidi kutumia muda wao kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji, michezo ili kujenga afya ya roho na mwili, wajifunze kuonesha ukarimu, utu wema na uwajibikaji. Kwa njia hii likizo itakuwa ni fursa kweli kwa vijana kukua kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.