Kardinali Fernando Filoni ,aliyetumwa na Papa Francisco kwenda Iraki, kwa lengo la
kuwa karibu na kushikamana na wateswa wa madhulumu yanayofanywa Iraki na makundi ya
Waislamu wapiganaji “wanajihad”, Jumatano alitembelea eneo la Erbil ya Kurdistani
ya Iraki. Kardinali kwa upendo na huruma kubwa alisalimia na kukumbatiana na makundi
ya watu walioacha nyumba zao wakiwa mikono mitupu kutoka eneo la ukanda wa Ninive.
Katika mahojiano na Sergio Centofanti wa Redio Vatican ,juu ya hali halisi
ilivyo baada ya kutembelea kambi kadhaa za wakimbizi hao, alisema, jambo la kwanza,
amesalimiana n akukumbatiana na mamia ya watu waliokusanyika kila mahali katika eneo
hilo , si tu katika bustani za jengo la Askofu, lakini pia waliopata mahali pa kuweka
kichwa, ndani ya jengo la Kanisa na shuleni pia. Kuna mamia kwa mamia ya watu waliokusanyika
hapo. Na hivyo, kazi ya kwanza kwa Kanisa, imekuwa kuwapokea na kuwafanikisha kuishi
watu hawa walio katika hali ngumu na hatarishi. Kwa bahati wakati huu si kipindi
cha baridi, ingawa kuna joto kali lakini bado ni ahueni kuliko kuwa nje kwenye baridi
kali. Na ndani ya majengo walau kuna kiyoyozi na hasa sehemu walikowekwa watoto.
Na nyakati za usiku watu wanaweza kulala nje ambako hewa ni mwanana. Na kwamba mipangilio
ya kuwaweka watu hao katika eneo ndogo inakwenda vizuri, kuna wema na fadhila nyingi.
Aidha Kardinali Filoni, akiitazama hali ya kisiasa, baada ya kukutana na kuzungumzana
uongozi, akiwemo Rais wa Mkoa wa Kurdistan, Rais Mas’ud Barzani , ameona kwamba,
wako tayari kutoa msaada na wameonyesha kujali ombi la Baba Mtakatifu la kupokea wakimbizi
hawa, na kuhakikisha, wanapata mahitaji msingi kimaisha. Na si kimaisha tu lakini
hata katika mambo mengine muhimu kwa mfano jinsi ya kusaidia wanafunzi waliokatisha
masomo yao , wengine wakiwa katika vipindi cha mitihani, upatikanaji wa huduma ya
tiba na dawa na uwepo wa utaratibu mzuri wa kusimamia na kugawa misaada ili wote waweze
kupata mahitaji yao msingi. Kardinali anaeleza kwamba , baadhi ya kambi wameamua kuwa
na jiko moja na wanajenga mabafu na vyoo vya muda, na pia wanajaribu kusaidia baadhi
ya familia ziweze kupangisha nyumba.
Na kwamba, aliwasilisha msaada uliotolewa
na Papa kwa Askofu mahalia ambaye ametoa kwa wahitaji kupitia taratibu zilizopo, na
kwamba watu wameonyesha shukurani kubwa kwa Papa si kwa ajili tu ya msaada wa kihali
lakini zaidi ya yote, kwa kupaza sauti yake kukemea madhulumu yanayowaweka watu
katika hali hizi ngumu . Katika eneo hili la Arbil, kuna wakimbizi karibia 160 elfu
kati yao, wakiwemo Wakristo na waamini wa madhehebu mengine madogomadogo .
Katika
mahojiano hayo, Kardinali Filoni, aliieleza hali halisi ya usalama katika eneo hili
kwmba bado ni tete. Na inaona bado kuna matatizo ya kuweza kutetea usalama wa nchi
na watu wake. Na hivyo kwa hilo , Kardinali ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa,
kutoa msaada wake si wa vitu tu lakini hasa msaada wa kisiasa na kijeshi. Utawala
unaona kuwa ni jambo nyeti sana kuomba msaada kwa jumuiya ya kimataifa. Na pia kwa
wakati huu serikali ya Kurdistan haioni kama ni jambo lazima sana kufanya hivyo kwa
wakati huu.
Kardinali Filoni anasema, pamoja na mahitaji yote hayo ya kihali,
pia kuna kiu ya kiroho na kisaikolojia kwa watu wengi. Na hivyo anatumaini kwa msaada
wa kihali unaotolewa kwa watu wote katika siku hizi uwezeshe pia kutoa utulivu wa
kiroho na kisaikolojia, wakati watu hao watakapoweza kurejea makwao.