2014-08-15 12:14:17

Kanisa ni mbegu ya umoja katika Familia ya binadamu!


Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2014, Baba Mtakatifu Francisko alipata chakula cha mchana na wawakilishi wa vijana kutoka Barani Asia wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya sita ya Vijana Barani Asia.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna vijana elfu sita kutoka katika nchi mbali mbali Barani wanaoshiriki katia siku ya sita ya Vijana Barani Asia inayoongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia".

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, vijana 18 wameshiriki chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. Hili nalo limekuwa ni tukio la furaha kwani vijana wamepata nafasi ya kumshirikisha Baba Mtakatifu maisha na utume wa Parokia zao na kumwalika kutembelea nchi zao. Kwa pamoja wameimba wimbo wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani pamoja na kupiga picha za kumbukumbu!

Baba Mtakatifu katika tafakari yake kwa vijana hawa wanaokumbatiwa na Mama Kanisa kutoka katika kila kabila, lugha na jamaa, anasema kwamba wao ni kielelezo cha uwepo wa Roho Mtakatifu anayefanya yote kuwa mapya, kama Yesu mwenyewe alivyowawezesha Mashahidi wa Korea kung'ara kwa njia ya ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; hawa ni mwanga unaoliangazia Bara la Asia, changamoto kwa vijana nao kuwa ni nuru katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, Kristo anawaita kuangalia katika maisha mambo msingi, kutembea katika barabara na njia za dunia huku wakibisha hodi katika milango ya watu ili waweze kumfungulia na kumpokea Kristo katika maisha yao. Kongamano la Vijana Barani Asia ni kielelezo cha mpango wa Mungu kwamba, hata Kanisa nalo linaitwa kadiri ya mpango wa Mungu kujenga misingi ya amani na urafiki; kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano; kwa kujenga na kuimarisha umoja; kwa kukataa katu katu uhalifu na hali ya kudhaniana vibaya.

Kanisa ni mbegu ya umoja katika Familia ya binadamu. Kwa njia ya Kanisa Watu wa Mataifa, Lugha na Jamaa wanaitwa kujenga umoja unaotambua utofauti, kwa kujikita katika upatanisho unaotajirisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, mwelekeo na mawazo ya walimwengu wengi ni tofauti kabisa na mwelekeo na mpango huu wa Mungu. Uadui na ukosefu wa haki ni mambo yanayotawala si tu kwa kuwazunguka watu bali hata kutoka katika undani wa mioyo yao; hali inayosababisha kinzani za kijamii; pengo kati ya maskini na matajiri; uchu wa mali, madaraka na anasa kupindukia; mambo ambayo yana gharama kubwa katika maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kuna watu ambao wamezungukwa na utajiri wa kupindukia, lakini kwa bahati mbaya ni maskini wa kutupwa katika maisha ya kiroho; ni watu wanaoelemewa na upweke hasi, ukimya na hali ya kukata tamaa. Hapa inaonekana kana kwamba, Mwenyezi Mungu hayupo tena katika hali kama hii. Hili ni jangwa la maisha ya kiroho linaloendelea kuenea sehemu mbali mbali za dunia anasema Baba Mtakatifu. Jangwa hili linawatendea sana vijana kwa kuwapokonya matumaini na hata zawadi ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kutoka kifua mbele kwenda duniani kote ili kuwatangazia watu Injili ya Matumaini, Injili ya Yesu Kristo, ili kuleta maisha mapya katika mioyo ya watu na kufanya mabadiliko katika medani mbali mbali za maisha, mahali ambako matumaini yamepotea. Huu ndio ujumbe ambao vijana wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha vijana wenzao: shuleni, katika maeneo ya kazi, kwenye familia, kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu na katika jumuiya zao.

Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ana maneno ya uzima wa milele na Neno lake lina nguvu ya kuweza kugusa moyo wa kila mwanadamu, kwa kushinda ubaya, kwa kuleta mabadiliko na kuikomboa dunia. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu, Yesu ameweza kuingia katika mioyo ya waamini kiasi cha kuwafanya kuwa kweli ni mashahidi wake mbele ya uso wa dunia.

Baba Mtakatifu anawauliza vijana ikiwa kama wako tayari kuwa kweli mashahidi wa Kristo Mfufuka na Injili ya Furaha kwa kujiaminisha katika nguvu ya Kristo; ukweli na neema, kwani vijana hawa kwa njia ya Ubatizo wameifia dhambi na kupata maisha mapya; wameimarishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi mioyoni mwao. Vijana wanapaswa kuwa karibu na Yesu kwa njia ya sala zao za kila siku.

Roho wake Mtakatifu atawasaidia vijana kufahamu na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Vijana wajichotee furaha na nguvu kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Moioyo ya vijana iwe safi pasi na mawaa kwa kujipatanisha daima na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kwamba, ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa uoneshe uhai na ukarimu wao. Licha ya giza na changamoto za maisha ya ujana, Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anawataka vijana kwa njia ya maneno, mawazo na matendo yao, daima yaongozwe na Neno la Kristo na nguvu ya ukweli. Vijana wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya Upadre na maisha ya Kitawa.







All the contents on this site are copyrighted ©.