2014-08-15 07:46:29

Iweni chachu ya mabadiliko duniani bila kumezwa na malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho sanjari na maadhimisho ya siku kuu ya uhuru wa Korea, Ijumaa tarehe 15 Agosti 2014 akiwa Jimboni Daejeon, Korea ya Kusini ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa kimataifa.

Baba Mtakatifu amekutana pia na kuzungumza na watu walioathirika katika ajali ya Meli iliyotokea hivi karibuni huko Sewol na kusababisha vifo vya watu 293, kati yao 10 hawajulikani waliko hadi sasa. Meli hii ilikuwa imebeba abiria 476.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo cha hatima ya watoto wateule wa Mungu na viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Anatambua nafasi ya Bikira Maria kama mwombezi na Mama wa Kanisa nchini Korea. Anamwomba ili aweze kuwakirimia ule uhuru waliojaliwa na Mama Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, ili aongoze juhudi zao katika mchakato wa kuleta mabadiliko duniani mintarafu mpango wa Mungu pamoja na kuliwezesha Kanisa kuwa ni chachu ya Ufalme wa Mungu nchini Korea.

Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria awawezeshe Wakristo nchini Korea kuwa kweli ni nguvu ya kuleta mabadiliko ya maisha ya kiroho katika medani mbali mbali. Wakristo wapambane dhidi ya malimwengu yanayotaka kumeza tunu msingi za maisha ya kiroho na kitamaduni, kwa kuchochea mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko ambayo hatima yake ni ubinafsi na kinzani.

Watu wawe na ujasiri wa kukataa mifumo ya elimu ambayo inasigana na utu wa binadamu, kiasi cha kusababisha umaskini, utengano wa wafanyakazi pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo usiothamini ile sura na mfano wa Mungu, chemchemi ya maisha; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Wakatoliki nchini Korea kutambua kwamba, wameitwa na wanapaswa kuthamini urithi wao, ili kuwa tayari kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Hii ni dhamana inayojikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuambatana na Neno la Mungu, kwa kushikamana na maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii.

Matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ni dawa tosha kabisa dhidi ya hali ya kukata tamaa, inayoendelea kujitokeza miongoni mwa watu kama Saratani. Jamii kwa nje inaonekana kuwa ni tajiri, lakini ndani yake inajikuta kwamba, ina ukakasi na utupu wa maisha. Hali ya kukata tamaa imewaathiri vijana wengi.

Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana amewakabidhi wananchi wa Korea chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, hasa wale waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye ajali ya Meli iliyotokea Sewol. Ajali hii ilikuwa ni alama ya mshikamano wa kitaifa katika majonzi, changamoto ya kuendelea kushirikiana kwa pamoja, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anawaweka chini ya ulinzi, usimamizi na maombezi ya Bikira Maria watu wote wanaoteseka hasa wagonjwa, maskini na watu wasiokuwa na fursa za ajira. Anamwomba Bikira Maria kuwafariji wale wote ambao bado wanaendelea kubeba makovu ya ukosefu wa haki wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baba Mtakatifu mwishoni, anawaweka vijana wote kutoka Barani Asia, wanaoadhimisha Siku ya sita ya Vijana Barani Asia chini ya ulinzi wa Bikira Maria. Anawataka wawe ni mwanga angavu wa dunia inayokumbatia amani kadiri ya baraka ya Mwenyezi Mungu.

Wakati huo huo, Askofu Lazzaro You Heung-sik wa Jimbo Katoliki la Daejeon katika hotuba yake ya shukrani amekumbushia hija za kitume zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili nchini Korea na mabadiliko yaliyojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi chote hiki. Kanisa Katoliki nchini Korea limejielekeza zaidi na zaidi kuwa ni Kanisa linaloshirikishana na wengine utajiri na rasilimali zake. Bado Korea inaogelea katika kinzani za kijamii na kisiasa, bado inawaombolezea watoto wake walizama na kufariki dunia baharini.

Katika mazingira magumu na tete kama yaliyoko kwa sasa nchini Korea, waamini wanafarijika kwa Neno la Mungu linalowachangamotisha kwa kuwaambia, ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia. Waamini wa Korea wanawaomba Mashahidi wa imani kutoka Korea waliopokea zawadi ya imani, wakaishi kwa upendo bila kuogopa kujisadaka katika maisha, wakawa tayari kumfuasa Mwalimu na Bwana wao Yesu Kristo, kwa kushuhudia imani katika matendo, wawe ni waombezi wao wa daima.

Askofu Lazzaro mwishoni anasema kwamba, kwa hakika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, wamesali Rozari Takatifu na kwa pamoja wamesali sala maalum kwa ajili ya maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu nchini Korea.







All the contents on this site are copyrighted ©.