2014-08-15 11:42:23

Huruma ya Mungu iwasukume watu kuguswa na mahangaiko ya jirani zao!


Kongamano la Kimataifa la Huruma ya Mungu ni kati ya urithi ambao Mama Kanisa ameachiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli, kwa waamini na watu wenye mapenzi mema daima kukimbilia katika huruma na upendo kwa Mungu kwa waja wake. Kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 19 Agosti 2014 kunafanyika Kongamano la kimataifa la huruma ya Mungu huko Bogotà, nchini Colombia. Kongamano hili linafanyika wakati kuna changamoto nyingi zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa.

Bado dunia imegubikwa kwa vita na kinzani za kijamii, kisiasa na kiuchumi; kuna mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kwa misingi ya kidini na kikabila; kuna vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu; vitendo vunavyosababisha majanga na maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna baa la njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato.

Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Huruma ya Mungu. Amani ya kweli haitaweza kutawala duniani ikiwa kama watu hawatakimbilia huruma ya Mungu na kujitahidi kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu ndani ya Kanisa.

Huruma inawawezesha watu kuguswa na mahangaiko ya jirani zao; kuonesha toba na wongofu wa ndani; kujikita katika upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu; kuwa wakarimu tayari kuwatendea wengine haki na ukarimu kwa kuonesha unyenyekevu na majitoleo kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Fadhila ya huruma iwasukume watu kuona na kuonja shida za jirani zao, tayari kuwafungulia malango ya imani, matumaini na mapendo.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, kumbe, huruma hii inawagusa watu wa dini na imani mbali mbali wanaokiri uweza na makuu ya Mungu katika maisha yao anasema Monsinyo Chidi Denis Isizoh, Afisa kutoka katika Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Watu wanaweza kuishi kwa amani na maridhiano ikiwa kama huruma ya Mungu itamwilishwa katika uhalisia wa maisha na kwamba, Yesu Kristo ni sura halisi ya huruma ya Mungu kwa binadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.