2014-08-14 11:16:10

Salam na matashi mema kutoka kwa Papa Francisko kwa wakuu wa nchi mbali mbali!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kichungaji kuelekea Korea ya Kusini, amebahatika kuruka katika nchi ya Italia, Croazia, Slovenia, Austria, Slovakia, Bielorussia, Russia, Mongolia na China.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais Giorgio Napolitano wa Italia anasema kwamba, anaelekea nchini Korea ili kuwapelekea ujumbe wa matumaini. Anamtakia Rais Napolitano na wananchi wote wa Italia maendeleo ya kiroho na kimwili. Amewatakia wananchi wanaoishi katika nchi zote zile ambazo amebahatika kupitia wakati anaelekea Korea ya Kusini amani na maendeleo.

Katika salam na matashi mema, Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anapita kwenye anga la China, amemtumia salam Rais wa China na kuwatakia wananchi wa China, heri na baraka zake za kichungaji.

Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa shukrani wakati alipokuwa anaelekea nchini Korea ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya VI ya Vijana Barani Asia. Rais Napolitano anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaifuatilia hija ya kwanza ya kitume Barani Asia kwa shauku kubwa kutokana na hali tete inayojionesha kwa sasa.

Ni matumaini yake kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unaojikita katika udugu na mshikamano utasaidia kugusa nyoyo za watu ili kujenga misingi ya amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.