Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa
mjini Seoul amepokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Korea ya Kusini, itifaki
ikiwa imezingatiwa. Vikosi vya ulinzi na usalama vilipiga mizinga ishirini na moja
kama alama ya kumkaribisha Baba Mtakatifu nchini Korea.
Baba Mtakatifu siku
ya Alhamisi asubuhi tarehe 14 Agosti 2014 kwa saa za Korea ameadhimisha Ibada ya Misa
Takatifu na sehemu kubwa ya mahubiri yake yamegusia kwa muhtasari hija yake ya kitume
nchini Korea ya Kusini.
Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka kuelekea
nchini Korea ya Kusini kwa ajili ya hija yake ya kitume, Jumatano asubuhi, tarehe
13 Agosti 2014 alikwenda kusali kwa faragha kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu
lililoko mjini Roma, ili kuiweka hija yake ya kitume nchini Korea, chini ya ulinzi
na usimamizi wa Bikira Maria. Akiwa Kanisa hapo, Baba Mtakatifu aliweka shada la maua
kwa Sanamu ya Bikira Maria.
Akiwa njiani kuelekea Nchini Korea ya Kusini, Baba
Mtakatifu alipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari ambao wako katika msafara
wake. Kwa pamoja wamesali na kumwombea mwandishi wa habari Simone Camilli kutoka Italia
aliyeuwawa kwenye Ukanda wa Ghaza wakati akitekeleza kazi yake kama mpiga. Baba Mtakatifu
anasema, haya ni madhara ya vita.
Baba Mtakatifu amewashukuru waandishi wa
habari kwa huduma yao kwa kutambua kwamba, wakati wa hija hii ya kitume wanayo kazi
kubwa ili kuhakikisha kwamba, ulimwengu unahabarishwa kile kinachoendelea katika hija
yake ya kitume nchini Korea. Wakati wa kipindi cha kiangazi, kazi inakuwa na ugumu
wake kutokana na uwepo wa joto kali.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewahimiza
waandishi wa habari kuwa ni wajumbe wa amani, kwani kwa sasa kuna majanga mengi yanayoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, hali ambayo inatisha.