"Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti
anapita. Naye akapaza sauti akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie! Wale watu waliotangulia
wakamkemea wakamwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: Mwana wa Daudi,
nihurumie! Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake.
Yule kipofu alipofika
karibu, Yesu akamuuliza, unataka nikufanyie nini? Naye akamjibu, Bwana, naomba nipate
kuona. Yesu akamwambia, Ona! Imani yako imekuponya. Na mara huyo kipofu akapata kuona,
akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu (Lk 18:35-43).
Mwinjili
Luka anatusimulia jinsi huyu kipofu alivyoichukia hali yake ya upofu na hivyo kutafuta
msaada. Huenda alishahangaika sana kujitibia lakini ikashindikana, na ndipo akalipeleka
tatizo lake la upofu kwa Yesu naye anamtoa upofu wake.
Wapendwa sisi wote ni
vipofu wa mambo mengi. Bahati mbaya hatujaufahamu upofu wetu, na hivyo hautukerwi
na hali hiyo hata kutusababisha kutafuta dawa ya upofu wetu. Mara ngapi tunapata muda
wa kukesha bar, kuhudhuria vikao vya harusi, kutazama TV kwa muda mrefu, lakini tukakosa
muda wa kusali binafsi na katika familia. Au, kushindwa kwenda kanisani, kwenye jumuiya
ndogondogo na kufuatilia mafundisho ya Mungu kutokana na kukosa muda au kuchoka? Huo
ni upofu!
Mara ngapi tunatumia fedha nyingi kwa kununua vitabu vya hadithi,
kufurahia kusoma magazeti ya udaku, kusoma vitabu vya hadithi, lkn tukakosa pesa ya
kununuli Biblia (ambapo ungenunua mara moja kwa miaka mingi), kushindwa kusoma Biblia
na kusimuliana mafundisho ya Mungu? Huo ni upofu!
Ni mara ngapi tunachangia
fedha nyingi katika maharusi na sherehe mbalimbali (mtu anakuwa na kadi za kuchangia
harusi, kicheni pati n.k. hata nne kwa mwezi), lakini hatuwezi kuchangia elimu ya
watoto wahitaji na kuwa makanisani michango mingi hadi inaboa? Huo ni upofu!
Ni
mara ngapi tunakumbuka kununua vocha za simu zetu, kulipa bili za umeme, kulilia ving'amuzi
km Dstv, Startime Azam n.k, lakini tunajisahaulisha kulipa zaka kamili ili Mungu atuongezee
kipato chetu na kutuepusha na majanga? Huo ni upofu! Ni mara ngapi tunapenda kuwasaidia
"wasio na shida", kuwafurahisha marafiki kwa 'kuwazungushia' raundi za vinywaji, kuwahudumia
vimada, lkn wazee wetu, watoto wetu na familia zetu zinateseka kwa kukosa mahitaji
ya lazima ya kila siku? Huo ni upofu!
Ni mara ngapi tunapenda kuomba msamaha,
kuwasamehe marafiki zetu na watu wengine, lakini tunashindwa kutoa msamaha kwa wenza
wetu wa ndoa, kwa watoto wetu, familia zetu hata tunashindwa kuongea nao wakati tunaishi
nao nyumba moja? Huo nao ni upofu!
Sisi wote ni vipofu, wapendwa, tunaohitaji
uponyaji wa Mungu. Tumuombe Mungu atuponye upofu wa uelewa wetu ili tubadilike kutoka
kutenda na kuyapenda yale yasiyo na faida na thamani halisi ya maisha yetu na kuanza
kuona mwanga wa kweli katika kutekeleza wajibu zetu kwa Mungu, kwa kanisa, kwa wazazi
wetu, wenza wetu, watoto wetu, kwa wenye mahitaji muhimu katika jamii zetu na kutenga
muda kwa ajili ya maandiko Matakatifu, sala za familia, misa Takatifu na maongezi
ya kiipendo katika familia.