2014-08-14 11:44:36

Jubilee ya miaka 25 ya Masista wa Mitundu, Tanzania


Shirika la Masista wa Pendo wa Huruma wa Mtakatifu Vinsenti wa Paolo Mitundu, Tanzania linaadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu Shirika hili lilipoingia nchini Tanzania kutoka Austria. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 15 Agosti 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Singida. Ifuatayo ni historia fupi ya pilika pilika za kuanzishwa kwa Shirika hili nchini Tanzania.
Uwepo wa Shirika letu hapa Mitundu -Tanzania ni tunda la Upendo wa Masista wa Pendo la Huruma wa Mt. Vinsenti wa Paulo wa Innsbruck.
Hatua zake
Shirika letu lilianza kama Mission ndogo baada ya kuwasili Tanzania Masista wetu waasisi:, Sr. Celine Mittelberger na Sr. M. Relinde Kleber Novemba, mwaka 1981, Sr. M. Carmen Saxl mwaka 1982 na baadaye Sr. Waltraud Mahlknecht mwaka 1983, kwa lengo la kufanya kazi ya umisionari kwa kutoa huduma za jamii kama vile afya, huduma ya mama na mtoto na elimu bila kufundisha watu Habari Njema ya Ufalme wa Mungu kwa njia ya katekesi na mafundisho mengine ya dini.

Historia yatuambia kwamba mnamo mwaka Mwaka 1981 Sr. M. Carmen pamoja na Sr. M. Corona walifika Tanzania sehemu ya Puma kwa ombi la Sr. Maria Mama Mkuu wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Ulimwengu kwa ajili ya kuwafundisha wasichana namna ya kuwahudumia wagonjwa na akina mama wajawazito. Lakini waliona hapo siyo mahali pao. Kwa hiyo walihitaji kuondoka ili kurudi Ulaya. Lakini walipofika Arusha walikuatana na Padre Dominiko wa Jamii ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu akawapeleka Heka kuwaonesha mahali ambapo wangeweza kutoa huduma. Lakini hata hapo haikuwezekana.

Baada ya kurudi Ulaya Mapadre wa Damu Azizi ya Yesu chini ya uongozi na Padre Mario Dariozzi waliwaalika Masista wa Pendo la Huruma wa Mt. Vinsenti wa Paulo wa Innsbruck kufika kutoa huduma za kijamii katika moja ya Parokia ambazo wanatoa huduma katika Jimbo la Singida. Ndipo Sr. M. Carmen akifuatana na Sr. Alexia, Bwana Bernado Duelli na mafundi waashi wawili kutoka Italia aliwasili Tanzania ili kuanza Umisionari.

Tarehe 17/01/1982 walifika Parokia ya Itigi wakapokelewa na Padre Francesco Paroko wa wakati huo. Tarehe 19/01/1982 waliwasili Mitundu kuona eneo lao kwa mara ya kwanza na kuamua kujenga nyumba kwa ajili ya huduma walizokusudia kuzitoa.

Penye nia pana njia: Pamoja na kwamba mwanzo ulikuwa mgumu sana, Masista waasisi walimtegemea Mungu katika yote kama Abrahamu alivyomtegemea Mungu bila kujua itakuwaje mbele ya safari yake. Wao pia walianza kazi yao bila kujua itakuwaje baadaye. Walikumbana na changamoto mbalimbali kama vile:

Pamoja na ugumu huu walifanikiwa kumaliza nyumba moja.
Wakiwa wanaendelea na ujenzi walikabiliwa na tatizo la ukosefu wa gari kwa ajili ya kubeba mchanga na vifaa vingine vya ujenzi. Waliomba msaada kwa Hayati Mhashamu Askofu Benard Mabula wa Jimbo Katoliki Singida naye akawasaidia, (Raha ya milele umpe ee Bwana …. Astarehe kwa amani. Amina). Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida waliazima mashine ya kuchomelea vyuma na hatimaye walifanikiwa kuezeka nyumba ya pili. Wanasimulia kwamba, siku inayofuata mvua kubwa ilinyeesha (1983) na hapo walionja kwa namna ya pekee upendo wa Mungu, walitambua mapenzi ya Mungu kwao, kama asemavyo Mtakatifu Vinsenti wa Paulo: “Mambo ya Mungu huja yenyewe na hekima ya kweli ipo katika kufuata Maongozi ya Mungu hatua kwa hatua”.

Taabu na mahangaiko havikukomea hapo. Siku moja Sr. M. Carmen akiwa safarini toka Itigi aliharibikiwa na gari, akalazimika kutembea km zaidi ya 16 kwa miguu kutoka Kijiji cha Itagata hadi Mitundu akiwa amembeba Yesu wa Ekaristi Takatifu mikononi.

Masista waliendelea na ujenzi huku wakitoa huduma. Ili kuweza kutoa huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani kwa ufanisi walihitajika wasaidizi wengine. Ndipo tarehe 19/03/1985 kwa Maongozi ya Mungu aliwasili Mitundu msichana wa kwanza aliyeitwa Maria Kitiku kujiunga na Masista hawa. Siku hiyo hukumbukwa kama ishara ya neema ya Mungu - kuanzisha Shirika, ingawa tangu mwanzo Masista hawakuwa na lengo la kuanzisha Shirika hapa Tanzania.



Kama Mungu alivyomwambia Abrahamu: ‘‘Nitakufanya kuwa Baba wa Mataifa mengi” Mwa 17: 4. Masista wetu pia kwa imani waliyokuwa nayo kwa Mungu wamefanywa “MAMA” wa mataifa na makabila mengi. Tena jina lao si hilo tu bali wameitwa pia ‘‘WAASISI‘‘.
Kutoka mche mmoja mwaka 1989 mpaka sasa Shirika letu hapa Tanzania lina jumla ya:




Shirika letu halikuku a na kuongeza tu katika idadi ya wanachama bali hata katika hadhi: Mwaka 1996 Mission ndogo ya Mitundu ilipewa hadhi ya kuwa Region, wakati huo walikuwa Masista 18 jumla wazalendo pamoja na waasisi wetu.
Mnamo Julai 27, mwaka 2012 wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirika uliofanyika Makao Makuu ya Shirika Innsbruck nchini Austria, Region ya Mitundu ilipewa hadhi ya kuwa Provinsi ya Mitundu – Tanzania na kusimikwa rasmi hapa Tanzania tarehe 27/09/2013.
HUDUMA ZA SHIRIKA
Masista wetu wamekuwa mstari wa mbele kuratibu na kusimamia shughuli mbalimbali ambazo wameturithisha sisi pia. Shughuli hizo ni hizi zifuatazo:

SHUKRANI
Tunawashukuru waasisi wetu kwa kukubali mwito wa Mungu kufika kwetu na kutuletea Roho na Karama ya Watakatifu Vinsenti wa Paulo na Luise wa Marillac. Asanteni Masista wetu kwa moyo wenu wa majitoleo, kujituma kwenu, bidii na uvumilivu wenu. Jumuiya imekua na leo tunashangilia, Jubilee oyee!

Tunawashukuru wakubwa wetu huko Innsbruck na Provinsi zote za Ulaya na wafadhili mbalimbali kwa upendo wenu mnaotuonesha na kwa misaada mbalimbali mnayotupatia.

Tunalishukuru Kanisa la Tanzania kuridhia uwepo wa Shirika letu na kwa kuzitambua huduma zetu. Kwa namna ya pekee tunatoa shukrani za pekee kwa Hayati Askofu Bernard Mabula kwa kuwapokea Waasisi wetu katika Jimbo la Singida na kuwaruhusu kumsimika Mt. Vinsenti hapa Mitundu ili aendelee kutoa huduma kwa wahitaji kupitia sisi Masista wake.

Tunamshukuru pia Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Mapadre, watawa na waamini wote wa Jimbo la Singida kwa ushirikiano uliopo. Tunawiwa shukrani kwa ajili ya upendo na mchango mkubwa wa Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu katika kuanzishwa Shirika letu hapa Mitundu. Mungu azidi kuwabariki.

Tunawashukuru watu wote wa Mitundu na vijiji vya karibu kwa ujirani mwema. Tunaishi kwa ushirikiano mzuri. Katika matukio ya furaha na huzuni tupo bega kwa bega. Serikali ya Kijiji inatambua uwepo wetu na huduma tunazotoa. Tuendelee kushirikiana, kupendana, kuthaminiana na kuheshimiana.

Mwisho tunamshukuru aliye mwanzo na mwisho wa yote kwa kututunukia zawadi ya Shirika la Pendo la Huruma. Zawadi ambayo ni mapenzi yake na tunda la Roho Mtakatifu anayeongoza Shirika letu kupitia wakubwa wetu. Jambo la muhimu kwetu ni kutekeleza utume wetu tukiongozwa na neno la Baba Vinsenti lisemalo: „Unipe mtu wa sala naye anaweza yote“. Sala inachukua nafasi ya kwanza Malezi, kazi na kujituma ni jukumu letu wote wanavinsenti ili kuitunza vizuri zawadi yetu.
MUNGU LIBARIKI SHIRIKA LETU.








All the contents on this site are copyrighted ©.