Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amekipongeza chama cha kitume cha Meter kwa kujisadaka
kwa ajili ya: ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto, kwani watoto ni tumaini la Kanisa
na Jamii katika ujumla wake na kwamba, watoto ni matumaini ya Kanisa la Kristo.
Ni
kutokana na kuguswa na mahangaiko ya watoto ndiyo maana viongozi wa Kanisa wameendelea
kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Chama hiki cha kitume kwa ajili ya kuwalinda na
kuwatetea watoto, tangu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI
hadi wakati huu anapoongoza Papa Francisko!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI anamshukuru na kumpongeza Padre Fortnato Di Noto kwa kuchapisha kitabu ambacho
kimemvutia sana Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Hiki ni kitabu ambacho kina
mchango wa Makardinali 8 na Maaskofu 70 waliotuma ujumbe wao katika kipindi cha miaka
kumi iliyopita katika maadhimisho ya Siku dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto
wadogo.
Kitabu hiki, kadiri ya barua iliyochapishwa na Sekretarieti ya Vatican
kinaonesha urafiki mkubwa kati ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na Padre Fortunato,
kuhusu mwelekeo wa elimu nchini Italia. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anaendelea
kumtia shime, kusonga mbele katika mchakato wa majiundo makini na elimu nchini Italia.