2014-08-13 11:47:29

Tamko!


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini katika tamko lake linabainisha kwamba, dunia inaendelea kushuhudia madhara makubwa yanayosababishwa na kile kinachodaiwa kuundwa tena kwa Kaliffato, iliyopigwa rufuku kunako tarehe 29 Oktoba 1923 na Kemal Atarurk, muasisi wa Nchi ya Uturuki ya wakati huu. Hiki ni kitendo ambacho kinaendelea kupingwa na waamini mbali mbali wa dini ya Kiislam, lakini Jeshi la Jihadi bado linaendelea kufanya unyama kwa watu wasiokuwa na hatia.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linawaalika viongozi mbali mbali na watu wote wenye mapenzi mema kulaani vikali vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu; mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini; kwa kuwauwa watu na kuwatundika kwenye maeneo ya hadhara pamoja na kuwalazimisha watu kuongokea dini ya Kiislam.

Makundi makubwa ya watu yanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao, kwa vile vile tu ni Wakristo au Jumuiya ya Wayazida. Huu ni uharibifu mkubwa wa nyumba za ibada na urithi wa kitamaduni. Makanisa na Monasteri yanaendelea kunajisiwa pamoja na kuharibu utambulisho wa kidini, lengo ni kuwajengea watu hofu, ili waweze kuongoka au kukimbia ili kusalimisha maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema hakuna sababu ya msingi inayoweza kuhalalisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa misingi ya kidini. Vitendo hivi ni ukatili dhidi ya Mwenyezi Mungu na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wakristo na Waislam wanaweza kuishi kwa amani na utulivu pasi na mashaka yoyote yale na kwamba, katika miaka ya hivi karibuni majadiliano ya kidini kati ya Waislm na Wakristo yamekuwa na kuboreka zaidi.

Madhulumu na nyanyaso wanazofanyiwa waamini wasiokuwa wa dini ya Kiislam yanahitaji ujasiri na uwajibikaji hasa kutoka kwa viongozi wa dini ya Kiislam, watu wenye mapenzi mema na wale wanaojikita katika majadiliano ya kidini kuungana pamoja ili kulaani mauaji haya ya watu wasiokuwa na hatia.

Lengo ni kuonesha kwamba, kweli wanajali na kuguswa na mauaji pamoja na mateso ya watu wasiokuwa na hatia na kwamba, majadiliano ya kidini hayana budi kuendelezwa ili kudumisha misingi ya haki, amani na uhuru wa kidini. Viongozi wa kidini waungane na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanaodhulumiwa wanarudi tena katika maeneo yao.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linahitimisha tamko lake kwa kuunga mkono wale wote wanaosimama kidete kupinga vitendo vya kigaidi na wanaotaka kutumia machafuko ya kidini kwa mafao yao binafasi. Baraza hili linaungana na Baba Mtakatifu Francisko ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuasha tena katika mioyo ya watu kiu ya majadiliano na upatanisho na kwamba, vita inashindwa kwa njia ya amani na wala si jino kwa jicho!







All the contents on this site are copyrighted ©.