Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho!
Mpendwa mwana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Bikira Maria kupalizwa
mbinguni mwili na roho. Ni zawadi kwa Mama Bikira Maria anayokabidhiwa mwishoni mwa
maisha yake hapa duniani.
Sherehe hii
huja kila tarehe 15 ya mwezi wa nane kadiri ya kalenda ya kilturujia ya Kanisa Katoliki.
Tunaposherehekea kupalizwa mbinguni kwa Mama Bikira Maria tunashangilia, lakini pia
tunataka kukua katika imani katoliki ambapo tunakumbuka kuwa mama kanisa mnamo Novemba
1, 1950 katika mamlaka aliyokabidhiwa na Kristu, Baba Mtakatifu Pio XII katika ile
hati iitwayo Munificentissimus Deus, ambayo tunaweza kuitafsiri kama “Mungu Mkarimu”
alifundisha wazi na kwa milele kuwa Mama Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili
ili amzae Mwana wa Mungu, aliyempa Yesu Kristu damu yake ya kibinadamu, akaambatana
naye mpaka chini ya msalaba, amepalizwa mbinguni mwili na roho. Amepalizwa mbinguni
mwili na roho ikiwa ni tuzo toka kwa Bwana wetu Yesu Kristu.
Fundisho hili
la kupalizwa mbinguni mwili na roho, limefundishwa baada ya tafakari kina, kanisa
likinyanyua maombi yake kwa Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu wa ukweli, katika unyenyekevu
na udumifu na hivi ikafunuliwa wazi na Mungu mwenyewe kuwa Bikira Maria amepalizwa
mbinguni. Mpendwa msikilizaji, ni zawadi kwa kanisa, ni zawadi kwa kila mmoja wetu
na hivi kinachofuata baada ya kupokea zawadi hii ya imani, ni heri na vigelegele kwa
kwa kanisa takatifu mbele ya Mama Bikira Maria mtukuka aliye pia Mama wa Kanisa.
Mpendwa
mwana wa Mungu, kwa sherehe hii tunafurahia kushirikishwa kwa Mama Bikira Maria katika
utukufu wa mwanae Yesu Kristu Mkombozi pekee wa ulimwengu. Utukufu ambao mama huyu
ameushiriki tangu mwanzo kwa fumbo la umwilisho, yaani Yesu Kristu kutwaa mwili wa
kibinadamu kwa njia yake. Si hilo tu bali kupalizwa mbinguni kunaambatana na fumbo
la pasaka na hivi Bikira Maria anamsindikiza mwanae mpaka chini ya msalaba akishuhudia
mateso. Kwa namna hiyo basi Mwana asingeweza kumwacha mamaye aoze kaburini, lazima
amtuze zawadi hiyo ya kupalizwa mbinguni. Kumbe Kanisa linapiga vigelegele kwa sababu
ya kutukuzwa kwa Mama wa Mungu lililo tunda la ufufuko.
Katika kusherehekea
kupalizwa mbinguni kwa mama Bikira Maria yafaa kutambua na kujifunza kidogo upi ni
mzizi wa Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Ndiyo kusema tangu mwanzo Mungu aliweka
jambo hili katika mpango mathubuti. Tunaona katika kitabu cha Mwanzo, lile anguko
la wazazi wa kwanza yaani Adamu na Eva, ambao kwa njia yao kifo kinaingia duniani,
na mara moja tangazo la upendo toka kwa Mungu linatolewa kwa mwanadamu, likiwa ni
kandamizo kwa shetani kama tusomavyo “nitaweka uadui kati yako wewe na huyo mwanamke”
Mw 3:15 yaani nyoka aliyeleta anguko kwa wazazi wa kwanza anaambiwa atawekewa uadui
mkali na uadui huu utakuja kwa njia ya mwanamke.
Kwa vyovyote vile mwanamke
huyu asingeweza kuwa Eva kwa maana Eva na nyoka walifanya urafiki. Ni lazima awe mwanamke
mpya kabisa. Mwanamke huyu kadiri ya mafundisho ya mababu na walimu wa Kanisa ni Mama
Bikira Maria, ni Eva mpya, ni yule ambaye wokovu utaingia duniani kwa njia ya utii
wake wake kwa Mungu. Kumbuka maneno yake kwa malaika Gabrieli akisema, “nitendewe
kama ulivyonena” Na zaidi ya hilo uzao wake haiwezekani ukawa ni Adamu bali ni Adamu
mpya, na hivi Yesu Kristu Masiya atakayetangaza uadui dhidi ya kifo yaani utawala
wa shetani.
Kristu mshindi wa kifo, aliye Adamu mpya haachi kumshirikisha mama
kwa karibu katika vita dhidi ya kifo na kwa namna hiyo basi Yesu na Maria wako pamoja
katika uadui dhidi ya nyoka kielelezo cha mwovu shetani. Bikira Maria ni mkombozi
mwenza (co- redemptoris) na hivi kwa sababu Mkombozi Yesu Kristu anapokufa mara moja
kifo chake kinafuatwa na ufufuko, vivyohivyo mkombozi mwenza Mama Bikira Maria anapokufa
lazima kifo chake kifuatwe mapema iwezekanavyo na ufufuko kabla ya ufufuko wa wote
na hapa ndipo kuna kupalizwa mbinguni. Mantiki hii inakuzwa na mababu na walimu wa
Kanisa wakianzia pale katika Proto – evangelium kitabu cha Mwanzo sura ya 3 :aya ya
15, Kama tulivyokwisha sema hapo mwanzoni.
Katika Agano Jipya, Bikira Maria
anapokea salaam ya pekee toka kwa malaika Gabriel akimwambia “salaam Maria ewe uliyebarikiwa
na Mungu! Bwana yuko nawe” Lk 1:28. Salaam hii ni amkio la juu kabisa (par excellence)
lenye kuonesha kuwa tangu mwanzo wa maisha yake na hata mwisho hana doa la dhambi.
Na hivi hayuko chini ya utawala wa kifo kilicho tabia ya dhambi. Ni mkingiwa dhambi
ya asili na hivi kwa namna yoyote angepalizwa mbinguni mwili na roho.
Anaambiwa
umebarikiwa kuliko na kati ya wanawake wote, kumbe baraka yake haichangamani na baraka
za wengine. Baraka hii haiji tu bali anapewa kwa sababu amejaa neema tangu kuumbwa
kwake na kwa sababu hiyo uwepo wa Bwana ni mkamilifu katika yeye. Baraka aliyonayo
mama Bikira Maria ni kinyume na laana ya kale ya kurudi mavumbini kwa wazazi wetu
wa kwanza. Mw 3:19. Ndiyo kusema kama Kristu ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa
na Adamu, basi Maria ni mshindi dhidi ya kifo kilicholetwa na Eva.
Kwa ushindi
huu lazima Bikira huyu atuzwe zawadi ya kushiriki utukufu wa Mwanae kabla ya wanadamu
wengine wote, ndiyo kupalizwa mbinguni. Kupalizwa Mbinguni ni kuendeleza ushindi na
ni mlango wa kumfuasa Kristu kuingia mbinguni kwetu sisi tuliokabidhiwa kwake pale
chini ya msalaba. “mama tazama huyu ndiye mwanao”! Kamwe mama hatatuacha katika uvuli
wa machozi, lazima atatoa chozi la upendo kwa mwanae na tutapata ondolea na msamaha
wa dhambi.
Nani kama mama? Mpendwa unayenisikiliza, kwa kupalizwa kwa Mama
Bikira Maria mbinguni tunaona ujio wa shime kwa akina mama wote, na hivi tunashangilia
nafasi kubwa katika maisha ya akina mama wanayozawadiwa kwa ushindi wa Maria mama
mtukuka, tunda la kwanza la ukombozi.ni ushindi wa akina mama wote, ni ushindi wa
familia zote.
Mpendwa mwana Kanisa tunapoadhimisha sherehe hii tunawaombea
watawa wote wa mashirika mbalimbali waliojiweka chini ya ulinzi wa Bikira Maria mpalizwa
mbinguni. Washike imani katoliki, wampende mama Maria kwa heshima na uchaji wa juu
na zaidi wakue katika fumbo na fundisho hili la kupalizwa Mbinguni mama Bikira Maria.
Kwa namna ya pekee tunaalikwa pia kuwaombea Wamisionari wa Damu Takatifu ya
Yesu ambao tarehe hii ya 15 mwezi wa nane 1815 Shirika lao lilianzishwa na Mtakatifu
Gaspari na kuwekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria wa Damu Takatifu. Wamisionari hawa
wanafanya kazi katika mabara ya Amerika, Ulaya, Asia na zaidi sana Afrika katika nchi
ya Tanzania na Guinea Bissau. Wajibu na karama ni kutangaza upendo wa Damu Takatifu
ya Kristu iliyotolewa msalabani kwa ukombozi wa ulimwengu. Ninakusindikizeni kwa
tafakari hii nikikuombea baraka tele za Bwana katika maisha yako zinazomwagika na
kububujika kwa njia ya Bikira Maria mpalizwa Mbinguni, mama mtukuka juu ya wanawake
wote, malkia wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa Kwenu na Padre
Richard Tiganya C.PP.S.